Kocha KMC: Tatizo ni Aiyee, Msuva, Kapera

KOCHA Mkuu wa KMC, Jackson Mayanja, amewataja wachezaji wake Salim Aiyee, James Msuva na Ramadhani Kapera kuwa ndiyo sababu kupokea vipigo mfululizo katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

 

KMC wameanza mbio za ligi kwa kuchechemea mara baada ya kupoteza katika michezo miwili ya kwanza. Katika mchezo wa ufunguzi walifungwa 1-0 dhidi ya Azam FC Uwanja wa Uhuru, Dar, huku mechi ya pili wakifungwa 2-0 dhidi ya Coastal Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na kuwa timu ya kwanza kutoka Dar, kupoteza michezo miwili mfululizo msimu huu.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mayanja amesema umekuwa mwanzo mbaya kwao kwa kuwa wachezaji muhimu hasa katika eneo la ushambuliaji wapo nje ya uwanja kwa wiki kadhaa wakisumbuliwa na majeraha na kukiri kuwa kama kina Aiyee wangekuwa fiti huenda mambo yangekuwa tofauti.

 

“Ni mwanzo mbaya kwetu ambao nafikiri unasababishwa na kukosekana kwa baadhi ya wachezaji wangu muhimu katika eneo la ushambuliaji, Aiyee, Msuva na Kapera wapo nje kwa wiki kadhaa wakiuguza majeraha, nafikiri kama wengekuwa fiti mambo yangekuwa tofauti,” alisema Mayanja.

Wachezaji hao wote waliumia kwenye mechi dhidi ya AS Kigali ya Rwanda katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Toa comment