local

Balaa la Mchepuko Mke Afunga Mtaa, Zzua Timbwili, Adai Talaka!

By

on

Balaa la Mchepuko Mke Afunga Mtaa, Zzua Timbwili, Adai Talaka!

DAR: Balaa la mchepuko linapokuzukia kwenye ndoa yako, weee! Lisikie hivyohivyo, usiombe likutokee kama kijana Hamza Imam lilivyomtia aibu mtaani.  Hamza, mkazi wa Madafu Tandika jijini Dar es Salaam, Jumatatu wiki iliyopita haikuwa njema kwake, baada ya mkewe Farida Masingisa kuanzisha timbwili kwa mwanamke mwenzake aliyemtuhumu kuwa ni mchepuko wa mumewe.

MAMBO YALIVYOANZA

Inaelezwa na chanzo chetu kuwa, Farida na Hamza ambao wamezaa watoto watatu, walianza kuishi kama mke na mume tangu mwaka 2000 na ilipofika 2008, waliamua kufunga ndoa. Kama wasemavyo Waswahili huwezi kula muwa bila kuvuka kifundo, kidudu nuksi kiliingia kwenye ndoa hiyo mwaka 2017 pale suala la madai ya mume kukosa uaminifu lilipojitokeza.

FARIDA ANAFUNGUKA

“Kuna siku nilikwenda kumuona ndugu yangu mgonjwa aliyekuwa amelazwa Hospitali ya Muhimbili, baada ya kumjulia hali nikatoka, kwa kuwa mume wangu ni mwendesha bodaboda nilimpigia simu anifuate pale hospitali.

 

“Akaanza kunizungusha mara hivi na vile, kitu ambacho hakikuwa kawaida yake, baadaye kwa kuwa mimi ni mtu mzima, nilijua kuna kitu kibaya alikuwa anafanya. Aliporudi nyumbani nikaiba simu yake na kuanza kuipekua,” alisema Farida. Mwanamke huyo alidai kuwa wakati anaipekua alikutana na vitu vya ajabu (hakuviweka wazi) ambavyo alidai vilimhakikishia kuwa mumewe si mwaminifu kwenye ndoa yao.

 

FARIDA AANZA UKACHERO

Kutokana na matokeo aliyopata kwenye upekuzi wa simu ya mumewe, Farida alidai kumbaini mwanamke mmoja aliyemtaja kwa jina la Ivon Chuma kuwa ndiye anayemuibia mumewe. Hali hiyo ilimkera kwa muda mrefu na kusababisha ugomvi wa mara kwa mara kati yake na Hamza.

 

“Tuachane, tuachane,” zilianza kuwa nyingi kwenye ndoa hiyo kiasi cha kumfanya Faridi aamue kujiengua kwa mkewe kiaina na kuanza harakati mpya za kimaisha huku akidaiwa akirudi kwa mkewe kwa kubipubipu.

 

Hata hivyo, Farida alipotafakari chanzo cha mgogoro kati yake na mumewe alijiridhisha kuwa, kimetokana na ibilisi wa mchepuko na hivyo kuamua kumfungia kazi Ivon, lengo likiwa ni kumkomesha aachane na mume wake.

 

VIOJA VYAJITOKEZA

Wakati Farida akihangaika kumtisha na kumvizia mwanamke anayemtuhumu ‘kumteka’ mumewe kimahaba, ni kama alikuwa akikoleza moto, si mumewe wala huyo mwanamke waliomsikiliza. “Nikamwambia sasa kama amepata mwanamke mwingine si aniache; akawa hataki, anasema kila mwanamke ana uzuri wake,” alisema Farida.

UZALENDO WAMSHINDA FARIDA

Baada ya kuvumilia kwa muda mrefu, wiki iliyopita ibilisi wa shari alimpanda kichwani Farida na hivyo kuamua kumfungia kazi kikwelikweli Ivon kwa kumfuata mahali anakodaiwa kupangishiwa na mume wake.

 

“Kwanza nilianzia kwa Mjumbe wa Nyumba Kumi, nikamlalamikia kuhusu huyu mwanamke kunichukulia mume wangu, baadaye nikaona haitoshi nimfuate nikampe vipande vyake,” alisema Farida.

 

Kama ni vipande vilizidi ukubwa na kuwa vijiti maana timbwili alilomfanyia Ivon, Farida halikuwa la kitoto; mtaani wenye macho na masikio yao walianza kujitokeza kushuhudia sinema ya bure na kusikia mipasho na maneno yaliyojaa ‘shombo’ la kufa mtu.

 

“Kwa nini unanichukulia mume wangu? Wanaume wengine huwaoni? Mwanamke huna haya!” Ni maneno yaliyotoka kwenye kinywa cha Farida mfululizo ‘kumnanga’ huyo mwanamke aliyemtuhumu kuwa anamuibia mumewe.

 

MUME ATIA TIMU

Kwa kuwa kamera yetu ilikuwa eneo la tukio, ilimnasa Hamza akifika eneo la tukio huku akiwa na hasira kali akilenga kumshikisha adabu mkewe kwa madai ya kuwa anamtia aibu mtaani.

“Niacheni, niacheniii, huyu ni mke wangu niacheni nimtie adabu, hawezi kuniaibisha namna hii,” Hamza alifoka huku akiwa amevua shati ambapo wasamaria wema walikuwa wakimzuia asimdhuru mkewe.

 

MKE AOMBA TALAKA

Baada ya kuona kuwa haungwi mkono na mumewe, Farida aligeuza kibao na kuanza kumdai mumewe talaka huku akimpa maneno ya kejeli ambazo si busara kuziandika gazetini. Hata hivyo, baadaye zogo lilitulia lakini Hamza alipotakiwa na mwandishi wetu kuzungumzia tukio hilo hakutaka; naye mtuhumiwa Ivon hakuweza kuzungumza chochote kuhusu tuhuma za kuiba mume wa mtu.

Toa comment

Posted from

About erick

Recommended for you

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *