NEWS

Tumfurahie Miraj Athuman, tukimlilia Rashid Juma

By

on


NA AYOUB HINJO

ZIKIWA zimesalia takribani dakika 30 mchezo wa Simba dhidi ya Tanzania Prisons kumalizika, nilimwona Rashid Juma akiingia kuchukua nafasi ya Francis Kahata. Kusema kweli nilishangaa.

Si kama simfahamu Rashid, hapana, kushangaa kwangu kulitokana na mawazo yaliyokuwa yakipishana kwenye kichwa changu mara kwa mara. Nilijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.

Mara ya mwisho kumwona uwanjani ilikuwa katika michezo ya kirafiki waliyocheza Simba walipokuwa Kigoma, dhidi ya Mashujaa FC na Aigle Noir huku akiwa ametoka kutoa pasi safi ya bao la Ibrahim Ajib dhidi ya Bandari FC ya Kenya. Nayo ilikuwa mechi ya kirafiki.

Ni nani asiyemfahamu Rashid hivi sasa? Sidhani kama yupo kwa wafuatiliaji wa soka la Tanzania, kwa ufupi tu, ni mchezaji ambaye anasubiri mechi za kirafiki ili kupata dakika nyingi za kucheza.

Ngoja niwakumbushe jambo moja, katika wakati ambao kocha wa Simba alihitaji ladha tofauti kwenye eneo la ushambuliaji la kikosi chake, Rashid alitumika licha ya uwepo wa akina Emmanuel Okwi, John Bocco na Meddie Kagere.

Ni ngumu kumfananisha Rashid na hao watatu lakini alitumika kwa ajili ya watatu hao, alikuwa na jukumu la kutengeneza nafasi (space), uwezo wa kuwafanya wapinzani wafanye makosa, labda na kufunga mabao, japo hilo alikuwa la msingi sana kwake.

Rashid alikuwa na majukumu mazito, yaliyomwitaji mchezaji aliyekomaa akili na mwenye kujua kipi anakifanya uwanjani ili kutimiza majukumu yake ya msingi.

Rashidi Juma

Sikushangaa kuona Simba walifunga safari kwenda mpaka Iringa kumchukua Miraj Athuman aliyekuwa Lipuli FC. Mchezaji wao wa zamani, alikuwa hapo miaka mingi nyuma lakini alikosa nafasi.

Miraj ameingia moja kwa moja kikosini, sababu anaifanya kazi ya Aussems aliyompa Rashid msimu uliopita kwa ufasaha zaidi.

Miraj anafunga mabao, atoa asisti na kutengeneza nafasi. Ni mchezaji wa utofauti kando ya Ibrahim Ajib, Deo Kanda, Francis Kahata na Clatous Chama.

Ni kipenzi cha mioyo ya mashabiki wa Simba. Ni kama kuisikiliza sauti ya Nandy ikiyalalamikia mapenzi. Viungo vyote vya mwili hutulia Miraj anapokuwa uwanjani, sababu wanajua kuna kitu kinaenda kutokea, kama si kufunga, atatoa pasi au kufanya tukio la ajabu kwa wapinzani.

Ametengeneza kombinesheni na Meddie iliyozalisha mabao zaidi ya matano, amekuwa kipenzi cha mashabiki ghafla, kila mmoja alihitaji kumwona Miraj walipotoka suluhu dhidi ya Prisons.

Walihitaji kuona utofauti pale mbele kwa Kagere ambaye alizungukwa na Kahata, Chama, Shiboub na Ajib, kisha baadae kuingia Hassan Dilunga, Rashid na Kanda ambao hawakuweza kufanya maisha ya mashabiki wa Simba kuwa rahisi mitaani mpaka kwenye mitandao.

Ni rahisi kumwona Miraj uwanjani, kazi yake inawakuna mashabiki wa Simba, lakini katika wakati huu ambao tunafurahia uwepo wake, inabidi tumsikitikie Rashid.

Rashid hana uhakika wa namba kikosini, hapati dakika za kutosha ili kumrudisha kwenye matumaini ya kupambana, pengine hata nafsi yake inaishi kinyonge sababu yupo katikati ya kundi kubwa la wachezaji bora zaidi yake.

Dhidi ya Prisons alitakiwa kufanya kazi ya Miraj, lakini alishindwa, hakufika hata nusu, alitoa pasi za ovyo, alipoteza mipira kwa urahisi, haikujulikana aliingia kufanya nini.

Kuna mambo mawili ya kufanya kumsaidia Rashid, moja, nahisi lipo katika akili ya kila mmoja wetu. Hakuna kingine zaidi ya kutoka kwenda kucheza, sababu hawezi kupata dakika za kutosha ndani ya Simba.

Aende sehemu ambayo atakuwa na uhakika wa kucheza kila mechi, atarudisha hali ya kujiamini, atarudisha uwezo wake, kubwa zaidi atapata uzoefu.

Miraj alifanya hivyo, Dilunga aliamua hivyo wakati yupo Yanga, alihitaji kuwa na kesho bora. Yupo aliyewahi kusema bora kula ‘ugali mlenda’ kwenye amani kuliko ‘wali kuku’ kwenye vita.

Rashid anahitaji kukua kiakili, hilo haliwezi kumtokea akiwa Simba, haliwezi kumtokea akiwa mchezaji wa akiba ambaye hata benchi kuonekana ni nadra.

Mtazame Yusuf Mhilu aliyewahi kuwa Yanga, kijana mdogo ambaye anaitengeneza pepo yake katika kikosi cha Kagera Sugar.

Mhilu hakuwa na utofauti na Rashid wakati yupo Yanga, hakupata muda wa kucheza, alishindwa kukua kiakili, lakini kwa miezi sita ya karibu amekuwa mchezaji hatari.

Alikubali kutoka Yanga ili aitengeneze kesho yake, alienda Ndanda kwa mkopo, baada ya hapo aliekea Kagera Sugar. Rashid anaweza kukopi na kupesti tu, kutoka Simba si mwisho wa maisha.

Anaweza kurudi Simba kama Miraj au Dilunga ambao waliondoka kwenye timu hizo kubwa hapa Tanzania, lakini wamerejea kwa heshima zaidi. 

Kwa sasa, itakuwa ngumu hata kwa Aussems kumpa dakika za kucheza Rashid kwenye mechi muhimu kama Miraj atakuwa mzima. Itakuwa ngumu mno hilo kutokea.

Mbili, anaweza kukomaa kwenye kikosi cha Simba na kufanya kazi kubwa zaidi ya kumshawishi kocha ambayo imewezekana kwa Mzamiru Yassin.

Mzamiru ameibuka katikati ya kundi kubwa la watu wasiopewa nafasi, amekubali kuwa punda, anaubeba kila mzigo anapokuwa uwanjani. Atakaba na kushambulia. Bado atakimbia kila mpira uliopo, kutoa sapoti au kuharibu mipango ya wapinzani. Vyote anavifanya.

Amekuwa mchezaji wa kipekee kando ya akina Jonas Mkude, Sharaf Shiboub, Said Ndemla na Chama. Amechagua kuwa alivyo sasa, ndio maana haiwezi kukushtua ukimwona anaanza au kukaa benchi.

Siwezi kumpangia Rashid cha kufanya, lakini achague njia sahihi ya kupita kwa ajili ya maendeleo yake na soka la Tanzania hasa kwa wachezaji wazawa, kwa ajili ya kikosi cha Taifa Stars.

Pengine wasiwasi ni mkubwa zaidi juu ya kesho yake, sababu akitoka nje ya Simba, kwingine wapi ataishi vizuri iwe kwa kulala, kula au maslahi? Labda inamwogopesha.

Katika wakati huu ambao nafsi zetu zinamfurahia Miraj kwa kila anachokifanya, tuiache mioyo yetu ilie kwa ajili ya Rashid Juma.Source link

About erick

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *