Morrison: Nisipofunga Nitatoa Asisti Yanga SC

KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Mghana Bernard Morrison, ameahidi kuhakikisha anafunga mabao kwenye kila mechi na akishindwa basi atatoa pasi ya bao ili timu hiyo ishiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.

 

Morrison amejiunga na Yanga kwenye usajili wa dirisha dogo lililofungwa Januari mwaka huu, na mpaka sasa amecheza mechi tano, amefunga mabao matatu na asisti mbili kwenye michuano yote.

 

Akizungumza na Championi Jumamosi, Morrison ameweka bayana kuwa, anazijua changamoto za ligi ni kubwa, hivyo amejipanga kuhakikisha anaisaidia klabu hiyo kadiri ya uwezo wake ili afanikishe dhamira ya kuiona mwisho wa msimu ikishiriki kwenye michuano ya kimataifa.

 

“Siku zote unapohama klabu moja kwenda nyingine ugumu huwa haukosekani hasa ukilinganisha na ulikotoka, ukweli ni kwamba kila ligi ina uendeshwaji wake ila kwa ligi hii ni tofauti kidogo na nilikowahi kupitia maana kuna ushindani wa hali ya juu lakini pia changamoto ni nyingi zaidi.

 

“Nimejipanga kuhakikisha naifungia katika kila mchezo hasa pale tu ninapopata nafasi ya kufunga au kutoa pasi ya bao kwa wenzangu, nafurahia sana kukutana na wachezaji wenye mapenzi na moyo wa ushirikiano hivyo kwa pamoja naamini tutafanikisha malengo haya,” alisema Morrison.

Stori: Musa Mateja, Dar es Salaam
Toa comment