Wagonjwa wa Corona Waongezeka Kenya, Kenyatta Afanya Maamuzi

RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta, amethibitisha kisa cha tatu cha maambukizi ya virusi vya Corona na kuamuru shule zote za kutwa zifungwe kuanzia leo Jumatatu.

 

Shule za mabweni zimepewa  hadi Jumatano kuhakikisha wanafunzi wote wanarejea nyumbani kwao kwa sababu ya homa hiyo na vyuo vikuu na vile vya amali vimepewa hadi Ijumaa kuwapa nafasi wanafunzi wote kurejea kwao.

 

Pia amethibitisha kuwa watu wengine wawili wameambukizwa virusi hivyo nchini humo ambapo mmoja alikuwa ameambatana na aliyeambukizwa akiwa kwenye karantini hospitalini Kenyatta.

 

Wahudumu wa afya wanaendelea kuwashughulikia na kuwatibu walioambukizwa.

 

Kutokana na hali hiyo, wasafiri wanaotokea nchi za kigeni zilizoathiriwa na homa hiyo ya Corona wamepigwa marufuku kuingia  Kenya. Watakaoruhusiwa kuingia ni Wakenya na wageni walio na vibali rasmi tu. Wakenya wote watakaorejea nyumbani katika muda wa saa 48 zijazo watalazimika kujiweka kwenye karantini na kusalia ndani.
Toa comment