Aliyekuwa Mhasibu wa Tanroads Adaiwa Kujitwanga Risasi

MHASIBU wa zamani wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Ruvuma, Justin Rwendera amefariki akidaiwa kujiua kwa kujipiga risasi mdomoni akiwa nyumbani kwake.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa amesema alijipiga risasi jana asubuhi kwa kutumia bastola yake,” alijipiga risasi mdomoni na kutokea sikio la kushoto. Bastola alikuwa anaimiliki kihalali.”

 

Amesema siku ya tukio, Amida Mahamoud ambaye ni mpishi wa Rwendera alifika nyumbani kwa mhasibu huyo wa zamani wa Tanroads na kukuta mwili wake ukiwa kwenye kochi huku damu zikiwa zimetapakaa.

“Ile bastola ilikuwa chini, aliwapigia simu ndugu wa marehemu na kutoa taarifa polisi,” amesema kamanda huyo.

Amesema siku moja kabla ya kujiua, Rwendera alirejea nyumbani saa 11 jioni akiwa amekunywa pombe na kumkuta mtoto wa kaka yake, Raulian Bathomeo ambaye alimuomba aingie ndani kula.

Amesema baada ya kula Rwendera alitoka na kwenda katika zizi la ng’ombe na Bathomeo aliondoka kwenda nyumbani kwake ambako alipokea taarifa za kifo.

Maigwa amesema polisi walikuta bastola, risasi saba na ganda moja la risasi, “bastola inashikiliwa kwa uchunguzi, hakuna aliyekamatwa kutokana na tukio hili.”
Toa comment