Askari Polisi Kortini kwa Utakatishaji Fedha

WATUHUMIWA wanne akiwemo Askari Polisi, Emmanuel Mkilia wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu ikiwemo kuisababishia Mamlaka ya Jeshi la Polisi hasara ya Sh. Mil 798.

 

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Donald Mhaika mtaalamu wa TEHAMA, Abdi Ally na Mohyadin Hussein ambao ni wafanyabiashara.

 

Akiwasomea hati ya mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Salum Ally kuwa washitakiwa wametenda makosa yao kwa nyakati tofauti.

 

Wanadaiwa kuwa kati ya Machi 19 na Oktoba 18, 2013 walijipatia Sh. Mil 798 kwa kujifanya kuwa wanaweka mfumo wa taarifa za watuhumiwa waliokamatwa na ambao wanashikiliwa kwenye vituo nane na kutoa hati mbili ambazo zilionyesha vituo vinne vimeshakamilika.

 

Katika kosa la utakatishaji fedha, inadaiwa walilitenda kati ya Machi 19 na 18 Oktoba 2013, ambapo kwa pamoja wakiwa ndani ya jiji la Dar es Salaam, walijipatia mali wakati wakijua mali hiyo inatokana na kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

 

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Wakili Wankyo amedai kuwa upelelezi wa shauri hilo upo katika hatua za mwisho kukamilika.

 

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwani makosa yao ni ya uhujumu uchumi, hivyo wamepelekwa gerezani na kesi imehairishwa hadi Januari 20, 2020 ambapo itakuja kwa ajili ya kutajwa.

 
Toa comment