Aveva, Kaburu, Hans Pope Kuanza Kujitetea

27 0

Aveva, Kaburu, Hans Pope Kuanza Kujitetea

Aliyekuwa rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na wenzake wawili wataanza kujitetea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Novemba 20 mwaka huu.

 

Mbali na Aveva wengine ni aliyekuwa makamu mwenyekiti wa klabu hiyo Godfrey Nyange (Kaburu) pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili Zachariah Hans Pope.

 

Wakili wa Serikali, Silvia Mitanto aliieleza mahakama hiyo kuwa wanaomba tarehe ya kutajwa ili weweze kuendelea na rufaa waliokata katika Mahakama Kuu ya Tanzania ya kupinga maamuzi yaliyotolewa na mahakama hiyo kuwaondolea mashtaka ya utakatishaji wa fedha washtakiwa Aveva na Nyange.

 

Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alisema upande wa mashtaka kama mmekata rufaa mtaendelea lakini mahakama hiyo itaendelea na usikilizwaji wa utetez Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 20, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kusikiliza utetezi.

 

Katika rufaa hiyo Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini( DPP), amepinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwaondolea Aveva na Kaburu mashtaka ya utakatishaji fedha na kuwapa masharti ya dhamana.

 

Katika kesi hiyo, Aveva na Nyange walikuwa wakikabiliwaa na mashitaka tisa ambapo Septemba 19 mwaka huu mahakama hiyo iliwaondolea mashtaka mawili ya utakatishaji fedha kwa kuwa upande wa mashitaka ulishindwa kuyathibitisha.

 

Hata hivyo, Mahakama hiyo iliawakuta na kesi ya kujibu katika mashtaka saba ambayo ni kughushi, kula njama, matumizi mabaya ya madaraka, kutoa nyaraka za uongo, na kutoa maelezo ya uongo ambayo upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha.

 

Katika shtaka la kwanza, Aveva na Kaburu walikula njama ya kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka. Shtaka la pili Aveva na Nyange wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kuandaa fomu ya kuhamisha fedha Dola za Kimarekani 300,000 kutoka kwenye akaunti ya iliyoko benki ya CRDB Azikiwe kwenda kwenye akaunti binafsi ya Aveva iliyoko benki ya Barclays.

 

Shtaka la tatu linalowakabili Aveva na Nyange inadaiwa kwa pamoja walighushi nyaraka iliyokuwa ikionesha Simba inalipa mkopo wa Dola za 300,000 kwa Aveva kitu ambacho sio kweli.

 

Katika shtaka la nne Aveva katika banki ya CRDB anadaiwa kutoa nyaraka ya uongo ikionesha Simba wanalipa mkopo wa Dola za Kimarekani 300,000.

 

Shtaka la tano linawakabili Aveva, Kaburu na Hans Poppe ambao wanadaiwa kughushi hati ya malipo ya kibiashara wakionesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zina thamani ya Dola za Kimarekani 40,577 huku wakijua kwamba siyo kweli.

 

Katika shtaka la sita , Aveva anadaiwa kuwasilisha hati ya malipo ya kibiashara ya uongo kwa Levison Kasulwa kwa madhumuni ya kuonesha kwamba Simba wamenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.

 

Shtaka la mwisho Aveva, Kaburu na Hanspope wanadaiwa kuwasilisha nyaraka za uongo kuonesha kuwa Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za kimarekani 40, 577 Mwisho.
Toa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *