Baada ya Mondi Kutangaza Kumzimia Mimi Mars, Zuchu Hapatoshi!

14 0Baada ya Mondi Kutangaza Kumzimia Mimi Mars, Zuchu Hapatoshi!

KITENDO cha mwanamuziki kinara wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, kuweka wazi hisia zake za kimapenzi kwamba, anamzimia kinoma mwanamuziki mwenzake, Marianne Mdee ‘Mimi Mars’, kimeibua tafrani.

 

VITA MPYA

Kubwa lililoteka vilinge vya wapenda ubuyu wa mastaa wa Bongo, ni vita mpya ambayo imeibuka mitandaoni kati ya mashabiki wa Mimi Mars na wale wa mwanamuziki mpya wa Bongo Fleva, Zuhura Othman ‘Zuchu’ ambapo sasa hapatoshi mitandaoni.

 

Miezi kadhaa iliyopita, Zuchu alisainiwa kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) iliyo chini ya Diamond au Mondi na tangu hapo, wawili hao wamekuwa, wakidaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi, kutokana na ishara wanazozionesha kwenye staili yao ya maisha yaliyojaa mahaba tele.

 

Kabla ya kuibuka kwa sakata la Mimi Mars au Chuga Queen, baada ya Mondi kutengana na mzazi mwenzake, Tanasha Donna, mapema mwaka huu, walitajwa warembo wengi ambao wangerithi nafasi hiyo kwa Mondi wakiwemo Tessy Abdul ‘Tessy Chocolate’, Jacqueline Obeid ‘Poshy Queen’ na wengine, lakini mwisho wa siku kura nyingi kutoka kwa mashabiki wao, ziliangukia kwa Zuchu.

 

 

MONDI NA MIMI MARS

Mwishoni mwa wiki iliyopita, kupitia ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 10.7, Mondi aliposti video ikimuonesha Mimi Mars akiimba na kucheza Wimbo wa Cheche wa Zuchu aliomshirikisha Mondi, unaofanya vizuri kwa sasa, kisha chini akaandika maelezo ya kuchokoza jambo yanayosema; “Mi’ nakapendaga haka katoto…

 

Sema sijui hata timing naikoseaga wapi Mwana wa Dangote… Doh!” Katika posti hiyo, Mondi ambaye alifanya hivyo akiwa jijini Arusha ambako ni nyumbani kwa wazazi wa Mimi Mars, alimalizia kwa ‘kumtag’ mrembo huyo mwenyewe.

 

Tangu alipoanza muziki wa Bongo Fleva, Mimi Mars ambaye ni dada wa damu wa mwanamuziki wa kimataifa wa Tanzania Vanessa Mdee ‘V-Money’, hajawahi kuweka wazi mtu ambaye anatoka naye kimapenzi zaidi ya kuwepo tetesi za kutoka na msanii mwenzake wa Bongo Fleva, Omari Mwanga ‘Marioo’ ambazo wote walizikanusha.

 

KUNA KITU

Kwa kuwa Mimi Mars hakuwa ameiposti video hiyo kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, kuliibuka maswali kibao juu ya namna alivyoipata video hiyo, ambapo baadhi ya mashabiki walihitimisha kuwa kuna kitu kinaendelea kati ya wawili hao.

MIMI MARS VS ZUCHU

Katika mazingira kama hayo huku mwenyewe Mimi Mars akiwa kimya, wafuasi wake waliingia kwenye ukurasa wake wa Instagram, ambapo alikuwa ameposti video ya kusisitiza matumizi ya njia sahihi za uzazi ili kutimiza ndoto zake na kuliamsha dude dhidi ya Zuchu.

 

Wafuasi hao walijifanya kumpa taarifa kuwa amezimikiwa na Mondi, lakini hawakuishia hapo, bali walianza kumshambulia Zuchu kwa maelezo kwamba, anapaswa kumpisha mrembo huyo kwenye nafasi yake kwa Mondi.

 

“Mwambieni Zuchu aanue jamvi kwa Simba (Mondi) mwenye umalkia wake anakuja kukaa.

“Muda alioachiwa Zuchu unatosha, inabidi tu ampishe Chuga Queen (Mimi Mars).

“Kiukweli hata kuendana na Mondi, Zuchu alikuwa haendani naye, lakini kwa Mimi (Mars), Mondi amefika penyewe, tunamkabidhi mtoto na ulinzi getini tunamuwekea…(jina la mchekeshaji wa kiume Bongo),” ilisomeka sehemu ya maoni ya mashabiki lukuki wakimshambulia Zuchu ambayo mengine hayaandikiki gazetini.

MASHABIKI WA ZUCHU

Kwa upande wao mashabiki wa Zuchu, nao waliibuka kwenye kurasa tofautitofauti za udaku za Instagram, kisha kujibu mapigo kwa kumshambulia Mimi Mars kuwa, hana hadhi ya kuolewa na Mondi.

“Huyo Mimi Mars haendani kabisa na Simba (Mondi), levo zake ni akina…(anatajwa msanii mdogo wa Bongo Fleva.

 

“Huyo Mimi Mars atupishe, sisi tuna jambo letu na Zuchu pale kwa Chibu (Mondi) tarehe 2, mwezi ujao (siku ambayo Mondi alitangaza kufunga ndoa).

“Waache wanga waseme sana, lakini wajue Zuchu ndiye malkia wa Wasafi na anampa Simba (Mondi) vya kurithi na vya kigeni, wengine tupa kule,” ilisomeka sehemu ya maoni ya mashabiki wa Zuchu kwenye kurasa za Instagram.

 

NDUGU AMKARIBISHA MIMI MARS

Hata hivyo, mmoja wa ndugu wa Mondi aliyeomba hifadhi ya jina alisema kuwa, yeye anamkaribisha Mimi Mars kama ndiye wifi yake. “Mimi huwa sina kinyongo, yeyote nitakayeambiwa ndiye wifi yetu ambaye Nasibu (Mondi) amempenda, basi ninamkaribisha kwa mikono yote,” alisema mmoja wa ndugu wa Mondi.

MAMA D ATOA NENO

Kwa upande wake, mama mzazi wa Mondi, Sanura Kassim ‘Mama Dangote’ alipotakiwa kutoa neno juu ya mwanaye kumzimikia kimapenzi na Mimi Mars, alisema bado hajaona hiyo posti.

“Bado sijaona na sijaletewa huyo mtu kwa kweli,” alisema Mama Dangote ‘Kubwa la Maadui’.

MIMI MARS NI NANI?

Mimi Mars amezaliwa Juni 21, 1992 huko Paris nchini Ufaransa. Ni msanii wa Bongo Fleva, RnB na Pop. Pia ni mwigizaji, mshereheshaji na mtangazaji wa vipindi vya televisheni.

STORI SIFAEL PAUL, RISASI
Toa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *