Boniface Mgombea Aliyefanyiwa Umafia, Kupambana na Mkumbo

14 0Boniface Mgombea Aliyefanyiwa Umafia, Kupambana na Mkumbo

BONIFACE Jacob a.k.a Bonny, ni mgombea ubunge wa jimbo la Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Ni kijana ambaye alizaliwa Ubungo Kisiwani, na ni msomi wa chuo kikuu (UDSM) ana shahada moja ya ualimu na amekuwa katika siasa tangu akiwa chuoni.

 

Aliwahi kuwa diwani wa Kata ya Ubungo kwa miaka kumi na kisha akawa meya wa Manispaa ya Kinondoni kabla ya kugawanywa na kuwepo Manispaa ya Ubungo, ambako nako alifanikiwa kuvaa joho la umeya wa Ubungo, naye ni muasisi wa manispaa ya Ubungo na tayari ameandika kitabu kueleza walichokifanya.

 

Ni kijana ambaye anajua kujenga hoja, lakini kubwa katika uongozi wake katika jimbo; amefanya mengi mazuri ya kimaendeleo, lakini amejikuta akifanyiwa umafia wa kutisha ili apotee katika siasa.

 

Lakini waliomfanyia umafia huo, hawakujali kwamba barabara nyingi katika jimbo, alisimamia ujenzi wake.

Umafia huo ni kule kuzushiwa taarifa kwamba, alikuwa amefukuzwa katika chama na aliyedaiwa Katibu Kata wa Chadema Asheri Mlangwa, hivyo kupoteza kila kitu ukiwemo umeya.

 

Akizungumza na UWAZI alipoulizwa kwa nini hilo lilitokea, anasema Boniface:

“Muda mfupi baada ya kusambaa kwa barua ya kughushi iliyodai nimefukuzwa uanachama, nilikanusha taarifa za barua hiyo. Asheri Mlagwa hakuhusika kwa kuwa tayari alishaondoka katika uongozi wa kata hiyo.

 

“Nilishtushwa na barua hiyo ambayo bado chanzo chake hakijajulikana na nikasema mimi bado ni mwanaChadema na hakuna kikao chochote cha chama kilichokaa hata kunijadili tu,” anasema.

 

Akaongeza: “Waliingia mkenge walioghushi kwa sababu meya katika chama, anafukuzwa na Kamati Kuu na Diwani anafukuzwa na uongozi wa kanda, lakini kwa kuthibitishwa na Kamati Kuu ya Chadema. Kwa mujibu wa Katiba yetu, hatua za kumfukuza diwani au mbunge, hazihusiani moja kwa moja na uongozi wa kata, japokuwa unaweza kutoa mapendekezo ambayo yanapelekwa kwenye kanda na kwenye Kamati Kuu.”

 

Cha ajabu ni kwamba, katika barua iliyoonesha kuandikwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Aprili 2, 2020 yenye kumbukumbu KUMB:NA. CAB./74/216/01/07 kwenda kwa Mstahiki Meya, Boniface Jacob, ilimweleza kuhusu kupokea nakala ya barua hiyo ya kufukuzwa kwake uanachama na sehemu yake ilisema:

 

“Kutokana na barua hiyo kunitaarifu kuwa: Umefukuzwa Uanachama kuanzia tarehe 28/04/2020, nachukua nafasi hii kukutaarifu rasmi kuwa, umekoma kuwa Mjumbe wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa mujibu wa kifungu cha 39(2)(f) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mtaa sura ya 292 toleo la Mwaka 2015, ikisomwa pamoja na Kanuni ya 73(1)(e) na (f) ya kanuni za kudumu za Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo za Mwaka 2019.

 

“Kwa kuwa umekoma kuwa Mjumbe wa Halmashauri, pia umepoteza sifa ya kuwa Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kuanzia tarehe ya barua hii, hivyo unatakiwa kukabidhi ofisi pamoja na vifaa au mali yoyote ya Manispaa ya Ubungo ikiwemo gari kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo.”

 

Bonny anasema barua hiyo haikumtikisa japokuwa ilimshitua kwa sababu, alijua ni mchezo mchafu wa kisiasa wa wapinzani wake kwa kuwa walijua kwamba atagombea ubunge.

 

“Cha kushangaza ni kwamba, nilipokwenda kuchukua fomu ya kugombea ubunge, mkurugenzi wa manispaa alinipa, Hakusema kwamba mimi sio mwanachama wa Chadema,” alisema.

 

Anasema ilibidi Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kuingilia kati na kusema chama hicho hakijamfukuza Bonny na kwamba bado ni Diwani wa Ubungo ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Ubungo.

Mnyika alisema kuhusu hilo, chama hakijawahi kujadili suala lolote kuhusu Bonny, na Asheri Mlagwa aliyedaiwa kuandika barua ya kumfukuza Bonny, alikanusha kuhusika na barua hiyo.

 

Mnyika anasema: “Kiongozi wa kitaifa isipokuwa mwenyekiti na makamu mwenyekiti , mamlaka yao ya nidhamu itakuwa ni Kamati Kuu ya chama Mstahiki Meya kwa kuwa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama na mmoja wa madiwani, ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama.

 

“Lakini kwa barua hii, tumemweleza vilevile Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo kwamba, taratibu hata kama mstahiki Meya asingekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, kwa nafasi yake tu ya umeya, utaratibu wa kinidhamu unaongozwa na muongozo wa chama, ambapo chama kina muongozo wa kusimamia wabunge, halmashauri wakiwamo madiwani na viongozi wa vijiji na mitaa. Katika mwongozo huu, sehemu E inahusu hatua za kinidhamu kwa wabunge na mameya.

 

“Ambapo kwa hatua za kinidhamu za mameya, ni tofauti na hatua za kinidhamu za madiwani wa kawaida, mameya hatua zao za kinidhamu zimeelezwa katika kipengele cha pili I.”

 

Akaongeza: “Kinasema kama kwa mfano maana hadi sasa hatujapokea malalamiko yoyote juu ya mstahiki Meya Jacob na hata kama kungekuwa na malalamiko juu ya utovu wa nidhamu au tatizo lolote, inapaswa yafikishwe kwa Katibu Mkuu kwa maandishi ili yafikishwe kwenye kamati ya maadili ya taifa.”

 

Alisema kwa hivyo, kwa mwongozo huo hata kama asingekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema kwa nafasi yake tu ya umeya, masuala yake hayawezi kushughulikiwa na ngazi ya kata wala wilaya au ngazi ya kanda, bali yanapaswa kuwasilishwa kwa Katibu Mkuu.

 

“Na nimebaini kwamba, kinachotajwa kwenye barua ya mkurugenzi kuwa eti kuna kikao kimekaa cha kamati ya utendaji, ni jambo ambalo si la kweli na hakuna kikao chochote cha kamati kilichokaa cha Kamati ya Utendaji ya Kata kuhusu kujadili hatua za kinidhamu za mstahiki meya na tumethibitisha kwamba, ambaye anaelezwa kuwa amesaini barua, Asheri Mlagwa si Katibu wa Chadema wa Kata ya Ubunge na Katibu wa Chadema wa Kata anaitwa Ezekiel Miraji,” alisema Mnyika.

 

Boniface anasema aliwekewa pingamizi katika nafasi ya ubunge, lakini amepitishwa na tume ya uchaguzi na sasa anagombea na ameahidi kufanya makubwa kwa maendeleo ya jimbo akichaguliwa kuwa Mbunge, kwa sababu yeye ni muasisi wa Manispaa ya Ubungo, hivyo anajua matatizo mengi ya eneo hilo kuliko mgombea yeyote mwingine jimboni.

 

Mpinzani wake mkubwa katika ubunge, ni Profesa Kitila Alexander Mkumbo ambaye amewaahidi wapiga kura wa Ubungo kufanya kazi kwa nguvu ya kuwaletea maendeleo hata katika sekta ya miundombinu ya barabara, maji na elimu.

 

Huko nyuma, Mkumbo aliwahi kuteuliwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji tarehe 4 Aprili 2017, akitokea chama cha ACT Wazalendo, ambapo alikuwa mshauri wa chama.

 

Prof. Mkumbo aliwahi kufanya kazi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwanza kama Afisa Tawala kuanzia mwaka 1999 hadi 2003, ambapo baada ya hapo, alijiunga na kada ya taaluma.

 

Prof. Mkumbo alipanda katika ngazi mbalimbali za kitaaluma kutoka Mhadhiri Msaidizi mwaka 2003 hadi kuwa Profesa Mshiriki mwaka 2014. Akiwa mwanataaluma na moja ya wasomi wa jamii wanaojulikana ndani na nje ya Tanzania, Prof. Mkumbo amechapisha makala nyingi katika majarida ya kitaaluma.

 

Aidha, Prof. Mkumbo amefanya kazi nyingi za ushauri wa kitaaluma kwa mashirika mbalimbali ya kimataifa na kitaifa, pamoja na Serikali na katika chama cha ATC wazalendo.

 

Prof. Mkumbo ana Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Southampton, nchini Uingereza, na Shahada ya Uzamili katika Saikolojia ya Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shahada ya Kwanza katika Sayansi na Elimu (BSc. Ed.).

MAKALA; ELVAN STAMBULI, UWAZIToa comment

Posted from

Related Post

Kisa Jero; Wolper Azua Songombingo

Posted by - March 26, 2020 0
Kisa Jero; Wolper Azua Songombingo March 26, 2020 by Global Publishers KILA kukicha mjini hakuishi mambo, unaweza kusema hivyo! Unaweza…

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *