CCM Yamhoji Naibu Waziri Waitara

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara amezungumzia taarifa za na kuhojiwa na kamati ya maadili ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara kwa tuhuma za ukiukwaji wa maadili.

 

Pamoja na mambo mengine inadaiwa Naibu Waziri huyo amehojiwa kuhusu tuhuma za kufanya vitendo vinavyoashiria kuanza kampeni mapema ya kuomba uteuzi wa kuwania ubunge jimbo la Tarime Vijijini kupitia tiketi ya CCM.

 

Waitara mwenyewe amekiri kuitwa na kuhojiwa na kamati hiyo jana Jumatano, Machi 25, 2020; “Ni kweli nimeitwa na kuhojiwa na kwenye kikao cha maadili lakini siwezi kusema nilichohojiwa kwa sababu mwenye jukumu la kuzungumzia mambo hayo ni mwenyekiti wa kikao,” amesema Waitara.

 

Kiini cha kuhojiwa kwa Naibu Waziri huyo zilianza mwaka jana alipotangaza nia kugombea ubunge katika jimbo la Tarime vijijini ambalo kwa sasa mbunge wake ni John Heche (Chadema).

 

Utetezi wa Waitara

Kwa mara kadhaa, Waitara amekaririwa akitetea uamuzi wake wa kutangaza nia haujavunja kanuni na taratibu za CCM kwa sababu jimbo la Tarime Vijijini linaongozwa na mbunge kutoka chama cha upinzani.

 

“Ningekuwa nimetangaza nia katika jimbo linayoongozwa na mbunge kupitia tiketi ya CCM kweli ningekuwa nimekwenda kinyume; lakini Tarime Vijijini linaongozwa na mbunge wa Chadema. Majimbo ya aina hii tunaruhusiwa kufanya vurugu zisizo na madhara ikiwemo kutangaza nia,” amesema Waitara.

 

Ameaongeza kwa kuhoji; “Hivi hawa viongozi wa CCM ambao hivi sasa wanadai mimi kutangaza nia kunaleta mtafaruku Tarime walikuwa wapi wakati wa uchaguzi mkuu uliopita tuliposhindwa majimbo yote ya Tarime mjini na vijijini?”
Toa comment