CEO MPYA SIMBA AITEKA BIASHARA Sven amuahidi zawadi ya mabao

16 0


NA WINFRIDA MTOI

OFISA Mtendaji Mkuu wa klabu ya Simba, Barbara Gonzalez, ni kama vile ameiteka mechi ya leo ya Ligi Kuu Bara kati ya timu yake dhidi ya Biashara United itakayopigwa Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo unakuwa wa kwanza kwa Wekundu wa Msimbazi hao kucheza nyumbani msimu huu 2020/21, huku bosi wao huyo akitarajiwa kuwa jukwaa kuu akishuhudia mtanange.

Simba ilianza ligi hiyo kwa kucheza na Ihefu FC ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1  kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Mchezo wa pili kwa Wanamsimbazi hao ilikuwa dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro na kumalizika kwa sare ya bao 1-1, hivyo kujikusanyia alama nne katika michezo miwili.

Katika michezo yote hiyo, Wekundu hao wa Msimbazi, hawakuonekana kucheza kwenye ubora wao kama ilivyokuwa matarajio ya mashabiki wengi wa kikosi hicho.

Sababu kubwa aliyoitaja kocha mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, kuwa ni viwanja walivyotumia mikoani imewafanya nyota wake wasicheze kwa uhuru.

Hali hiyo pia ilimfanya kocha huyo kupanga wachezaji tofauti kulingana na mechi na aina ya uwanja, hivyo nyota wake muhimu kukaa benchi.

Katika mechi dhidi ya Ihefu FC, Sven alianza na Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein, Joash Onyango, Kennedy Juma, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin, John Bocco, Clatous Chama na Bernard Morrison.

Aliifanyia mabadiliko madogo kikosi kilichoanza dhidi ya Mtibwa Sugar akimuanzisha Luis Miquissone badala ya Dilunga. Licha ya kucheza pamoja na Miquissone, Morrison hakuweza kuonesha makali yake hadi kufikia hatua ya kutolewa kabla ya mechi kumalizika.

Katika mchezo wa leo, ile ladha ya Morrison kucheza pamoja na Miquissone inaweza kuonekana kutokana na uwanja wanaotumia kuwa mzuri na wameuzoea.

Aidha huenda kocha akatumia washambuliaji wawili, tofauti na mechi zilizopita ambapo alimtumia nahodha Bocco pekee yake.

Biashara United itashuka dimbani ikiwa imetoka kushinda mechi zake mbili mfululizo na kujikusanyia pointi sita.

Msimu uliopita Simba ilipokutana na Biashara United, ilianzia ugenini na kushinda mabao 2-0 katika dimba la Karume wakati katika mechi ya marudiano Uwanja wa Mkapa, Simba walishinda tena 3-1.

Kwa matokeo ya msimu uliopita, ni wazi Biashara United itakuwa imejipanga kufuta uteja kwa Wanamsimbazi hao, hivyo mchezo unatarajiwa kuwa mgumu kwa pande zote.

Kingine kitakachoifanya Simba kuhitaji zaidi matokeo ya ushindi, ni mechi yake ya kwanza kucheza nyumbani tangu msimu huu ulipoanza Septemba 6, mwaka huu.

Katika kuhitaji ushindi zaidi na kuwapa raha mashabiki wake, Wanamsimbazi hao waliamua kupunguza kiingilio na kuweka shilingi 3,000 kiwango cha chini, badala ya shilingi 5,000 ambacho kimezoeleka.

Mechi hiyo imeelezwa kuwa itakuwa ni rasmi ya kumkaribisha CEO mpya, Barbara, aliyepewa majukumu hayo hivi karibuni akichukua nafasi ya Senzo Mbatha alikwenda Yanga.

Kuelekea mchezo huo, kocha mkuu wa Wanamsimbazi hao, Sven, amesema kuna faida nyingi ya kucheza uwanja wa nyumbani, amefanya maandalizi mazuri ya kucheza soka la kushambulia.

Alisema katika mchezo huo, atamkosa Charles Ilamfya ambaye amepewa ruhusa ya siku tatu kushughulikia matatizo ya kifamilia.

“Tunacheza nyumbani matarajio yetu ni kucheza vizuri na kutafuta ushindi, kiufundi tumefanya maandalizi yatakayotupa matokeo mazuri,” alisema Sven.

Katika hatua nyingine, Sven alifunga mjadala wa Meddie Kagere kutokana na kuanzia nje tangu mechi za mwisho wa msimu uliopita na kusema ni suala la kiufundi, kati yake na mchezaji na hawezi kuliweka wazi.

Kwa upande wake, kocha mkuu wa Biashara United, Francis Baraza, alisema anapanga kikosi  cha ushindani kwa Simba kutokana na kufahamu ubora wa timu hiyo.Source link

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *