Corona Yachangia Ongezeko La Watu Kujiua

4 0Corona Yachangia Ongezeko La Watu Kujiua

Kujiua (Suicide) ni mojawapo ya vyanzo vya kifo kwa watu wenye matatizo ya kisaikolojia au matatizo ya akili. Jaribio la kujiua kwa mfano kunywa sumu au kujinyonga ni mojawapo ya dalili inayoonyesha kuwa mtu huyo ana tatizo la kisaikolojia au tatizo la akili.

 

Tatizo hili linakua kila siku duniani na Tanzania kwa ujumla kwa sababu tafiti za mwaka jana kutoka Shirika la afya duniani (WHO), zinaonesha kuwa wastani wa mtu mmoja duniani kila baada ya sekunde 40 hufariki dunia kwa kujiua.

 

Kwa upande wa Tanzania takwimu zinaonesha kuwa watu 16 kila mwezi hujitoa uhai kutokana na sababu mbalimbali hii ikiwa na maana kwamba kwa wastani, watu 200 hupoteza maisha kwa kujiua hapa nchini.

Hayo yanajiri katika kipindi hiki ambacho maambukizi ya virusi vya Corona yameathiri zaidi ya watu milioni 29 duniani na kusababisha vifo milioni moja.

 

Hata hivyo, Septemba 10 ambayo ni siku kimataifa ya kuzuia kujiua duniani, takwimu za mashirika mbalimbali duniani zinaonesha kuwa maambukizi ya Corona ambayo yalianza kusambaa Januari mwaka huu na kushika kasi Machi hadi Mei mwaka huu, nayo yamesababisha ongezeko la watu kujiua duniani.

 

CORONA YAZIDISHA WATU KUJIUA

Shirika la kimataifa linalojishughulisha na uzuiaji wa watu kujiua duniani (IASP) lililoanzishwa na Erwin Ringel na Norman Farberow mwaka 1960 na kuungwa mkono na Shirika la Afya Duniani (WHO), ndilo lililoasisi siku hii ya Septemba 10 kila mwaka kuwa siku ya kuzuia kujiua duniani.

 

Hata hivyo, katika ripoti ya IASP mwaka huu inaonesha kuwa maambukizi ya sio kwamba yanawaathiri watu kiuchumi pekee bali hata kiafya kwa upande wa kisaikolojia hali ambayo imesababisha wengi kujiua hivyo kulazimu shirika hilo kuunda Jumuiya ya utafiti wa kupinga kujiua kwa watu kipindi cha Covid-19 (ICSPRC).

 

Kwa mfano katika nchi ya Marekani, utafiti mpya unaonyesha kuwa huenda makumi ya maelfu ya wananchi wa Marekani wataaga dunia kwa kunywa pombe kupita kiasi, kubugia dozi zilizopitiliza za mihadarati au kujiua kutoka na msongo wa mawazo uliosababishwa na janga la corona.

 

Utafiti huo uliofanywa na Shirika la Well Being Trust likishirikiana na Akademia ya Madaktari wa Kifamilia ya Marekani (American Academy of Family Physicians) umeonesha kuwa, yumkini Wamarekani 150,000 wakajitoa uhai kutokana na kukata tamaa na msongo wa mawazo uliosababisha na athari za janga la corona.

 

Aidha, taarifa za Idara ya Taifa ya Takwimu ya Uingereza zinaonyesha kuwa, wakati wimbi la maambukizi ya virusi vya corona lilipofikia kiwango cha juu zaidi nchini humo, katika kipindi cha kati ya mwezi Aprili hadi Juni mwaka huu, viliripotiwa visa 845 vya watu waliojiua.

 

Kutokana na hali hiyo, Profesa Murad Khan ambaye ni rais wa shirika hilo la IASP anasema tatizo la watu kujiua linazidi kushika  duniani.

 

Anasema watu takribani 800,000 hufariki kwa kujikatiza uhai wao kila mwaka kwa mujibu wa Shirika la afya duniani (WHO) na ni sababu ya pili ya vifo miongoni mwa watu wenye umri kati ya miaka 15 na 29, nyuma ya vifo vitokanavyo na ajali za barabarani.

 

VIJANA  NDIO WANAOATHIRIKA ZAIDI

Kwa mujibu wa watafiti kutoka IASP na wataalam wa kisaikolojia wanadai kwamba wanaoathirika zaidi na tatizo hili ni vijana wenye umri kati ya miaka 15-29.

 

Rika hilo linaathiriwa zaidi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo hali za kubalehe. Pia kujihusisha na mapenzi, kutengwa na jamii, hali duni ya maisha na kukosa msaada huku takwimu ikithibitisha kwamba vijana wa kiume ndio wanaongoza kujiua kuliko vijana wa kike.

 

Vijana wengi wa kiume hujiua kwa sababu ya kuwa na maamuzi ya moja kwa moja yaani katika sababu moja ambayo inaweza kuwakumba vijana wa jinsia zote vijana wa kike wanaweza kukabiliana nayo tofauti na vijana wa kiume wanaoshia kukatiza uhai wao.

 

Aidha, Daktari bingwa wa magonjwa ya akili katika hospitali ya taifa nchini Tanzania (Muhimbili), Dk. Praxeria Swai anafafanua kuwa kuna sababu nyingi ambazo zinapelekea kundi la vijana hawa wanapelekea kutaka kujiua.

 

Anasema vijana wengi huwa ndio umri wa kubalehe na wanapitia changamoto nyingi, mara nyingi huwa wanajaribu vitu vingi sana katika maisha yao.

 

“Familia na vijana mara nyingi huwa wanakuwa hawaelewani, malumbano mengi, hawana taarifa sahihi na kile kinaweza kutokea na wanataka kujaribu kila kitu kama vilevi,” anasema.

 

UTAMJUAJE MTU ALIYEPO KATIKA HATARI YA KUJIUA?

Makamu wa kwanza wa rais wa shirika hilo IASP, Prof. Jane Pirkis anasema japo sio wote lakini watu wengi wanaotaka kujiua hutoa viashiria vifuatavyo; Huonyesha hali ya huzuni na kukata tamaa, hujiona mwenye hatia na aibu kwa mambo yaliyopita, hujaribu kujiua kila mara,  hujawa na mawazo kuhusu kifo lakini pia anaweza kuwa anatoa wosia au kuwaasa watoto au wengine kugawa vitu vyake n.k.

 

Pia  huwa na mabadiliko ya ghafla katika hali ya kujijali vilevile mabadiliko katika hamu ya kula na usingizi au kama ni mwanafunzi ufaulu waje husuka kwa kiasi kikubwa, kutoona umuhimu wa maisha ya baadae na hata kuandika au kuzungumzia kutaka kujiua.

 

SABABU ZA WATU KUJIUA

Wataalam wa afya kama vile Prof. Murad Khan na jopo lake wameeleza  kuwa kuna sababu nyingi zinazosababisha watu kujiua hasa katika kipindi cha Covid-19 ikiwemo hali ngumu ya kiuchumi, njaa, kutengwa kwa watu na mapenzi.

 

Vivyo hivyo wataalam na wanasaikolojia na viongozi wa dini kama vile Mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya maadili, amani na haki za binadamu kwa jamii ya viongozi wa dini, Askofu William Mwamalanga anaeleza kuwa sababu za watu kujiua ni pamoja na uvunjifu wa haki, ukosefu wa amani, mapenzi, umaskini, kufukuzwa kazini na msongo wa mawazo.

 

NINI KIFANYIKE KUZUIA WATU KUJIUA

Mtaalam wa masuala ya saikolojia Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk. Isack Lema anasema ni vyema elimu ikatolewa kwa jamii ili iweze kuwa na elimu pana kuhusu dalili na madhara ya watu kujiua.

 

Pia jamii itambue wajibu wa kila mtu ulimwenguni, kutambua thamani ya mwenzake na kuepuka uvunjifu wa haki na amani.

 

Aidha, Askofu Mwamalanga anaongeza kuwa ni wajibu wa viongozi wa dini kuendelea kuwafundisha watu kuwa na hofu ya Mungu na kutambua kuwa kujiua ni dhambi ambayo inapingwa hata kwenye vitabu vya dini.

 

Dk. Leman aye anaongeza kuwa watu wengi wanaojiua huonyesha dalili ambazo huashiria kutokea kwa hatua hii ya kujinyonga.

 

Anasema ikitokea wewe, ndugu au jamaa yako amejaribu kujiua, yawezekana ikawa ni kiashiria kua mtu huyu yupo katika hatari ya kupata ugonjwa wa akili au matatizo ya kisaikolojia. Ni vizuri ukampeleka hospitali akapatiwa uchunguzi na msaada wa kisaikolojia kutoka kwa wataalamu wa afya na magonjwa ya akili.

 

Kwa sababu tafiti zinaonyesha kua endapo mtu ana mawazo ya kutaka kujiua, au alishawahi kujaribu kijiua, uwezekano mkubwa ni kua siku moja atafanikiwa kujiua kweli. Hivyo natibabu ni muhimu.

Mashauri Samwel na Susan Manyauli, TUDARCoToa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *