Dybala wa Juventus Nimepona Corona

PAULO Dybala amewaambia mashabiki wa timu yake ya Juventus kuwa kwa sasa afya yake na ya mpenzi wake, Oriana Sabatini ziko safi ikiwa ni siku nne tangu aweke hadharani kuwa ana Virusi vya Corona.

 

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 aliwashitua mashabiki wengi wa soka baada ya kujitangaza kuwa na virusi hivyo ambavyo ni tishio kwa sasa, kiasi cha kusababisha michezo mingi na shughuli nyingine nyingi kusimamishwa.

 

Akitumia ukurasa wake katika Instagram aliandika:

“Sasa tuko vizuri” huku akiweka picha akiwa anaonyesha dole gumba.

Juventus, ndiyo ilikuwa klabu ya soka kubwa ya kwanza nchini Italia kutangaza juu ya mchezaji wake kuambukizwa virusi hivyo ambaye ni Daniele Rugani baadaye akafuatia Blaise Matuidi kisha Dybala.

 

Baada ya kugundulika wakiwa na virusi hivyo Dybala na mpenzi wake waliamua kujitenga kwa kukaa ndani kwao muda wote huku wakipatiwa matibabu.

 

Italia imeathirika kwa kiwango cha juu na virusi hivyo ambapo kuna watu zaidi ya 74,000 wametajwa kuambukizwa Corona huku zaidi ya 7,500 wakifariki dunia.
Toa comment