Eric Shigongo: Maoni Yangu Kuhusu Corona

18 0

Eric Shigongo: Maoni Yangu Kuhusu Corona

MARA nyingi nimeongea na watu ninaofanya nao kazi kwanba sifa ya kiongozi bora ni kuwa na uwezo wa kulitatua tatizo kabla halijatokea; mfano rahisi ni njaa, baba mwenye hekima huweka akiba ya chakula pale tu anapoona kuna uhaba wa mvua au nchi imevamiwa na nzige.

 

Pale nchi hiyo itakapoumbwa na njaa kutokana na ukame familia yake iliyotakiwa kufa na njaa itapita salama watoto wakisema “Sisi kwetu hatukuiona njaa” bila kufahamu baba yao alilitatua tatizo kabla halijatokea.

 

USISUBIRI MPAKA NJAA IKUFIKIE NDIO UANZE KUWEKA CHAKULA.

Donald Tump, rais wa Marekani alisikia juu ya CORONA ilivyokuwa inaua wachina akiwa bado hajapata hata mgonjwa mmoja, akaonywa kwamba ugonjwa huu ungesambaa dunia nzima, kiongozi huyu wa taifa kubwa lenye nguvu kifedha, alibaki bila kufanya maandalizi akiuita ugonjwa huo “Chinese virus.”

 

Leo hii Marekani inaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa Corona duniani, wamarekani zaidi ya 2000 mameshapoteza uhai wakati nchi hiyo haikuwa hata na mgonjwa mmoja.

 

Si rahisi kuamini kwamba Hata vifaa vya kuhudumia wagonjwa katika jiji la New York havitoshi, wauguzi wanakosa hadi maski!!!!!! Hii ni aibu kubwa kwa taifa kubwa kama Marekani, Trump alishindwa kutumia pesa kujiandaa kabla tatizo halijatokea, leo anatumia dola trilioni 2 kuwagawia watu wake wanaokufa ili kufufua uchumi. Hii ni aibu ya karne.

 

Nchi za Afrika ikiwemo Tanzania ambayo mpaka sasa ina wagonjwa 14 haijapoteza hata mtu mmoja huku Misri ikiwa na wagonjwa 576, Morrocco 358, Africa kusini 1187 na Algeria 454 zinapaswa kujifunza kutoka kwa Trump, zisifanye makosa kabisa, zitatue matatizo yajayo mbele kabla hayajatokea na huu ndio uwe utaratibu wetu.

 

Viongozi wa Afrika wafanye juhudi kudhibiti maambukizi kabla hayajakuwa makubwa hata kama itahitaji gharama kubwa kwani Kama ugonjwa huu unaisumbua Marekani na China, sisi itakuwaje? Ni heri Kinga kuliko tiba wahenga walisema.

 

Kamwe nchi za Afrika zisisubiri mpaka tatizo litokee na kubwa ndio maandalizi yaanze, yafanyike mapema yasitukute ya Trump, gharama itakuwa kubwa na tutapoteza maisha ya watu wengi na uchumi tunaoujenga utaporomoka hadi zero.

 

Raia wa Afrika nasi tunapaswa kutii na kufuata maelekezo ya wataalam wetu ili kuuepuka ugonjwa huu na kuepuka kuambukiza wengine.

 

Nionavyo mimi tukiyafanya haya tutakuwa tumedhibiti tatizo kabla halijatokea ama kudhibiti madhara kuwa makubwa kabla hatujakutwa na aibu kama ya trump. Huo ndio uongozi bora.

 

Asanteni sana ndugu zangu,
Mungu ibariki Afrika,
Mungu ibariki Tanzania.

Shigongo, Eric James.
Dar es Salaam.
Toa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *