Harmonize Atibuliwa Kila Kitu

DAR: Kwa sasa adui namba moja wa dunia ni Virusi vya Corona ambavyo vinasababisha maradhi ya COVID-19.

Janga hilo halijamuacha salama staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ kwani limemtibulia kila kitu.

 

Kufuatia Serikali mbalimbali duniani kupiga marufuku mikusanyiko na ziara za kimuziki, Harmonize au Harmo anasikilizia maumivu ya kushindwa kufanya ziara zake ambazo alikuwa anatarajia kuzifanya ili kutangaza albam yake ya Afro East aliyoizindua hivi karibuni pale Mlimani City jijini Dar.

 

Katika mahojiano maalum na Gazeti la IJUMAA, meneja wa Harmo, Beauty Mmari ‘Mjerumani’ alisema kuwa, jamaa huyo alikuwa na ziara ya kuitangaza Afro East, lakini imeshindikana kwa sababu ya kusambaa kwa Virusi vya Corona duniani.

 

“Tulikuwa na tour (ziara) ya Albam ya Afro East, lakini kutokana na janga la Virusi vya Corona, tumelazimika kusitisha kila kitu.

“Ilikuwa tutembelee mikoa na nchi mbalimbali, lakini hatuwezi hadi hali itakapokuwa sawa.

 

“Kufuatia janga hili, Harmonize anaungana na Watanzania wengine na watu mbalimbali duniani kuhamasisha kujikinga na Corona na kumuomba Mwenyezi Mungu atujalie hili nalo lipite kama mengine ambayo yalishapita.

 

“Ninaamini tutavuka, kikubwa naendelea kusisitiza kuwa tuwe tunasikiliza mamlaka husika ambayo ndiyo yenye dhamana katika kututangazia na sisi tufuate maelekezo,” alisema Beauty.

Albam ya Harmo ina nyimbo 18 ambazo ameshirikiana na wanamuziki kibao wa ndani na nje ya Bongo.

 Stori: NEEMA ADRIAN, Ijumaa
Toa comment