Israel, Falme za Kiarabu sasa mambo safi, Netanyahu anaamini hatua hiyo itamaliza uhasama 

9 0

Rais wa Marekani Donald Trump ameongoza sherehe ya kuwekeana uhusiano wa kibalozi kati ya Israel, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain, akiimarisha nafasi ya kuchaguliwa tena mwezi Novemba.

Akizungumza wakati wa kuyasaini makubaliano hayo katika Ikulu ya White House mjini Washington, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameisifu hatua hiyo, akisema inaweza kuwa mwanzo wa kumaliza kabisa uhasama wa muda mrefu kati ya nchi yake na ulimwengu wa kiarabu.

Amesema ilikuwa siku ya kihistoria inayoashiria mapambazuko mapya ya amani, na kusema hatua ya amani waliyopiga leo, itadumu. Netanyahu ameelezea matumaini yake, kuwa mfano wa Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu utafuatwa na nchi nyingine za kiarabu.

Waziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Abdullah bin Zayed al-Nahyan, binafsi amemsifu Netanyahu, ambaye amesema amechagua amani kwa kusitisha unyakuaji wa ardhi za Wapalestina.

Historia yachukuwa mwelekeo mpya

USA Washington Weißes Haus | Abkommen Naher Osten (Reuters/T. Brenner)Sherehe ya kuyasaini makubaliano hayo imefanyika katika Ikulu ya White House mjini Washington

Rais Donald Trump ambaye kusainiwa kwa makubaliano haya ni muhimu kwa sera yake ya nchi za nje huku akielekea katika uchaguzi wa mwezi Novemba, amesema historia ya Mashariki ya Kati imebadilisha mkondo.

”Baada ya miongo ya mgawanyiko na mizozo, tunafikia mapambazuko mapya kwa Mashariki ya Kati. Shukrani kwa viongozi jasiri wa nchi hizi tatu, tunapiga hatua kubwa kuelekea mustakabali ambapo watu wa dini na asili tofauti wataishi pamoja kwa amani na ustawi.” Amesema Trump.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanasema mafanikio kutokana na makubaliano haya ni madogo, kwa sababu uhusiano kati ya Israel, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu umekuwa mzuri kwa muda mrefu, na nchi tatu hizo zina mtazamo sawa wa kuipinga Iran.

Wapalestina wasema wamesalitiwa

Kwa upande mwingine, Wapalestina wameyapinga makubaliano yaliyosainiwa mjini Washington, wakisema ni usaliti ambao hautasaidia mchakato wa amani.

Kiongozi wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas amesema tatizo lililopo sio kati ya Israel na nchi mbili za kiarabu zilizohusika, bali na Wapalestina ambao ardhi zao zinakaliwa kimabavu.

Saudi Arabia imetoa tangazo la kuwaunga mkono Wapalestina, na kusisitiza kuwa amani ya kudumu itapatikana kwa kuundwa taifa huru la Wapalestina katika mipaka ya mwaka 1967, mji wake mkuu ukiwa Jerusalem Mashariki.

Iran na Uturuki pia ziliyalaani makubaliano hayo hata kabla ya kusainiwa. Spika wa baraza la wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi amesema bunge linahitaji kujua zaidi undani wa makubaliano hayo.

Hayo yakiarifiwa, duru kutoka Ukanda wa Gaza zimearifu kuwa ndege za Israel zimeushambulia ukanda huo, baada ya wanamgambo wa Hamas wanaoudhibiti kurusha kombora lililowajeruhi watu wawili kusini mwa Israel.

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *