Jarida la Yanga Laja na Neema Kibao

UONGOZI wa Klabu ya Yanga chini ya Mwenyekiti Dk.Mshindo Msolla, jana Alhamisi ulizindua jarida la klabu hiyo linalohusu mambo mbalimbali ya klabu ambapo limeambatana na neema kibao kwa mashabiki wa Yanga.

 

Jarida hilo lenye kurasa 48 litakuwa likiuzwa kwa bei ya shilingi 5,000 ambapo litauzwa nchini kote kupitia matawi mbalimbali ya Yanga yaliyozunguka nchi nzima.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mwenyekiti Msolla alisema kuwa jarida hilo limetengenezwa kwa niaba ya mashabiki wa timu hiyo kwa ajili ya kulisoma ili kufahamu mambo mbalimbali yanayoihusu timu hiyo, na kwa ambao watanunua jezi za timu hiyo katika maduka ya GSM, watalipata jarida hilo bure.

 

 

“Jarida letu hili tumeliandaa kwa ajili ya kuwaelimisha mashabiki wetu mambo mbalimbali yaliyotokea zamani na sasa, ambapo jarida hili litapatikana kwa Sh 5000 tu ila kwa wale ambao watanunua jezi za Yanga katika maduka ya GSM watalipata jarida hili bure kabisa,” alisema.

 

Aidha kwa upande wa michakato mbalimbali ya kimfumo wa mabadiliko, ujenzi wa uwanja na mchakato wa ubadilishwaji wa katiba ya klabu hiyo, Msolla alisema vyote vimesimamishwa mpaka pale kamati tendaji itakapotangaza tena kutokana na uwepo wa maambukizi ya Ugonjwa wa Covid-19.

 

“Kutokana na uwepo wa Ugonjwa wa Covid-19 ambao ni hatari sana kwa afya zetu, tumeona tusitishe michakato yote kuanzia ule wa ubadilishwaji wa klabu kimfumo wa uendeshwaji, uundwaji wa katiba mpya na ule mchakato wa ujenzi wa uwanja wetu kule Kigamboni mpaka pale kamati tendaji itakapotangaza tena,” alisema mwenyekiti huyo.

Stori: Marco Mzumbe | Dar es Salaam
Toa comment