Joash Onyango: Nitawakomesha Wanaoniita Mzee

BEKI wa kati mpya katika kikosi cha Simba, Joash Onyango ambaye ni raia wa Kenya, amesema kuwa amesikia kuna baadhi ya watu wamekuwa wakibeza muonekano wake na kumwita mzee, sasa wasubiri kwani atawakomesha.

 

Onyango aliyejiunga na Simba kwenye dirisha hili la usajili kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Klabu ya Gor Mahia ya Kenya, alizua tafrani kubwa kwenye mitandao kutokana na muonekano wa sura na ndevu zake ambazo hapo awali alizipaka rangi nyeupe kiasi ha mashabiki kumtania kuwa ni mzee.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Onyango alisema ni kawaida kwa mashabiki kusema kile wanachojisikia hivyo suala hilo amelizoea na halimpi shida.

 

“Yah ni kweli nimesikia baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiniita mimi mzee kutokana na muonekano wangu, jambo hilo wala halinipi shida kwa sababu ni hali ya kawaida na wala halibadilishi uhalisia wangu, lakini nadhani wameona nilichokifanya dhidi ya Vital’O.

 

“Nitaendelea kujituma na kucheza kwa kiwango cha juu zaidi ya kile nilichokionyesha ili kuwakomesha na kuwaziba mdomo wale wote wanaoniita mzee,” alisema Onyango.Toa comment