Kagere, Chama Wazua Balaa Simba SC

BALAA kubwa huenda likawakumba baadhi ya wachezaji wa kimataifa wa Simba kutokana na kudaiwa kukiuka taratibu za klabu hiyo.

Wachezaji hao ni Mnyarwanda, Meddie Kagere, pamoja na Mzambia, Clatous Chama.

Kwa pamoja wachezaji hao wanadaiwa kukiuka taratibu za timu hiyo baada ya kuondoka nchini hivi karibuni na kwenda makwao bila ya ruhusa ya uongozi wa timu hiyo.

 

Wachezaji hao wanadaiwa kuwa walijiamulia wenyewe kuondoka nchini baada ya uongozi wa timu hiyo kutoa mapumziko ya siku saba kwa wachezaji wote ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wengine wa klabu hiyo baada ya ligi kusimama kutokana na Virusi vya Corona.

 

“Baada ya kupewa mapumziko hayo, uongozi uliwataka kubaki hapa nchini lakini wao waliamua kuondoka bila ruhusa jambo ambalo siyo sawa.

“Ruhusa walizokuwa nazo hapo mwanzo zilikuwa za kwenda kujiunga na timu zao za taifa kwa ajili ya michuano ya kimataifa, lakini baada ya tishio la Corona michuano hiyo iliahirishwa na tulipokea barua kutoka katika nchi zao wakituambia kuwa hawawahitaji tena wachezaji hao.

 

“Kwa hiyo kutokana na hali hiyo walitakiwa kubakia hapa nchini kuendelea na taratibu walizokuwa wamepewa na benchi la ufundi, lakini wao wakakaidi na kuamua kuondoka.

 

“Kwa hiyo, kutokana na hali hiyo lazima tuwachukulie hatua za kinidhamu kwa kukiuka maagizo ya timu,” alisema kiongozi huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini na kongeza:

 

“Mchezaji ambaye anaweza kupona kati ya hao waliopo nje ya nchi ni Shiboub (Sharaf Eldin) peke yake kwa sababu yeye aliondoka mapema kabla ya kutolewa kwa taarifa za kusitishwa kwa michuano hiyo.”

 

Alipotafutwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa ili azungumzie hilo hakupatikana.

Stori na Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam
Toa comment