Kikwete: Kuibiana Kawaida, Yanga Achaneni na Morrison Mnapoteza Muda

8 0Kikwete: Kuibiana Kawaida, Yanga Achaneni na Morrison Mnapoteza Muda

 

RAIS Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Jakaya Mrisho Kikwete ambaye pia ni shabiki kindakindaki wa Klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam ametoa rai kwa vilabu vya soka nchini kuwekeza kwa vijana huku akiwataka Yanga kuachana na mchezaji aliyekuwaklabu hiyo na sasa amekwenda Simba Bernad Morrison.

 

Kikwete amesema hayo leo Agosti 30,2020 katika Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam ambapo Klabu ya Yanga wana jambo lao la Siku ya Wananchi ambalo pamoja na mambo mengine huitimishwa kwa kutambulisha wachezaji wake, benchi la ufundi na viongozi.

 

Katika Siku hii ya Wananchi maelfu ya wananchi wamejitokeza uwanjani hapo kushuhudia burudani mbalimbali na kisha kuchezwa mechi ya kirafiki kati ya timu ya Yanga na timu ya Aicle Noir CS ya kutoka nchini Burundi.

 

Akizungumza mbele ya mashabiki, wapenzi na wanachama wa Yanga Kikwete amesema amefurahishwa na jinsi ambavyo idadi kubwa ya mashabiki wa klabu hiyo wamejitokeza uwanjani hapo.”Hongereni sana,kumefana na kumbe mkiamua mnaweza sasa nawataka muamue ligi ijayo mpate ubingwa.

 

“Hakuna lisilowezekana, mliweza miaka mingi iliyopita na katika miaka mitatu hii ubingwa umewaporonyoka, mnaweza kuirudisha. Nguvu ya umoja nimeiona,leo mmeonesha kumbe mnaweza kutokuwa baridi,” amesema Kikwete.

Hata hivyo wakati akiendelea kuzungumza Mzee Kikwete amewaambia Yanga kwamba kwa sasa kuna maendeleo yanayoonekana katika klabu hiyo. “Miaka michache iliyopita hali ilikuwa mbaya,mnapeleka timu Mbeya mnatembeza bakuli.

 

“Mlifanya uamuazi tukakutana ukumbi wa Diamond jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mchango kuendesha shughuli za Yanga. Nilialikwa na kwa ukereketwa wangu nikaja, lakini watu wawili Rostam Azizi na Gharib Mohamed wamekuwa msaada mkubwa kwa klabu yetu.

 

“Rostam tunafahamiana miaka mingi tangu vijana mpaka sasa tunazeeka. Nilifurahi sana alipoulizwa na Rais ni timu gani akajibu mimi Yanga. Tukaenda kwenye ule mchango Rostam akanipigia simu akasema atachangia shilingi milioni 200.

“Natoka wakati ule ndugu zetu wawili hawa ndio wametuondolea unyonge Yanga, kama sio ndugu zetu wawili hawa yule mchezaji maarufu wangempataje na sisi tumezoea kuibiana tu, tubakwenda kuiba Simba na safari hii nao wameiba,” amesema Kikwete.

 

Amefafanua kuwa hayo ndio maisha ya Simba na Yanga yalivyo ya kuibiana wachezaji na haikuwa kwa Morrison tu bali ni enzi na enzi. “Huko nyuma tulikuwa na mchezaji na Simba wakamuiba, alikuwa mazoezini Yanga na alipotoka hakurudi tena na sisi Yanga tukachukua mchezaji wa Simba.

 

Ushauri wangu wekezeni kwa vijana, tunzeni vipaji, kuna umuhimu wa timu ya watoto, huko nyuma tulikuwa na timu ya watoto ndio wakapatikana wachezaji akina Sande Manara.

 

“Wekezeni kwenye katika timu za watoto na hili ni kwa timu zetu zote iwe Simba, iwe Azam, ifike mahali hakuna sababu ya kwenda kutafuta wachezaji nje na badala yake tuwekeze kwenye vijana wetu,” amesema Kikwete na kuwataka Yanga kufahamu kuchukuliwa kwa Morrison sio jambo jipya.

 

Ametumia nafasi hiyo kumpongeza na kumshukuru Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga Profesa Mshindo Msolla kwa kumtaka kuendeleza umoja na mshikamano ndani ya Timu yao.

 

” Nakupongeza sana Prof Mshindo wewe ni kiongozi msomi, umewahi kuwa kocha na sisi kama Yanga tunategemea ujenge umoja na mshikamano kwani kwenye umoja halishindakani jambo lolote.

 

“Nawashukuru GSM ni matumaini yetu mtaendelea kuwa pamoja na nasi, Abbas Tarimba nakushukuru kwa Spotpesa, na sasa na unakednda kwenye ubunge sijui utaacha, kama utaendela tutashukuru.

 

“Muwe na ushindani wa uhakika na hiyo itatokana na uwekezaji katika michezo,tafuteni walimu wazuri kwa ajili ya kuisaidia timu, nawaombea mpate ushindi,” Amesema Kikwete.Toa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *