Kisa Jero; Wolper Azua Songombingo

13 0

Kisa Jero; Wolper Azua Songombingo

KILA kukicha mjini hakuishi mambo, unaweza kusema hivyo! Unaweza kuamini kuwa staa anaweza kuanzisha songombingo kisa shilingi 500 ‘jero’? Risasi Mchanganyiko lina habari ya dizaini hiyo.

 

Iko hivi; msanii wa filamu za Kibongo, Jacqueline Wolper juzi kati alizua timbwili la aina yake baada ya kugoma kulipa ‘Jero’ ya maegesho.

 

ILIKUWAJE?

Chanzo chetu kilieleza kuwa, mwishoni mwa wiki iliyopita, msanii huyo alikwenda kwenye duka lake eneo la Sinza jijini Dar es Salaam akiwa na gari lake aina ya Toyota Alphad na kupaki nje ambapo mtoza ushuru wa Tarura (Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini) alifika na kumuwekea risiti ya kulipia jero ya maegesho ambayo hata hivyo Wolper aligoma kulipa.

 

“Wolper alikataa kulipa kwa sababu alidai lile ni eneo lake la biashara na huyo mtoza ushuru wa Tarura alisema gari lilikuwa kwenye hifadhi ya barabara inayomilikiwa na serikali, hivyo msanii huyo alitakiwa kulipa ushuru kwa mujibu wa sheria za Tarura.

Aidha, baada ya msanii huyo kugoma kulipa, aliondoa gari kwa nguvu na kumwacha mtoza ushuru akipigwa na butwaa.

Inaelezwa kuwa mtoza ushuru hakuwa na cha kufanya zaidi ya kurejea ofisini kwao na kutoa taarifa.

 

TARURA WATINGA

Siku iliyofuata, timu ya Tarura ilifika eneo analofanyia biashara Wolper na kukuta amepaki gari lake kama kawaida, ambapo walilifunga tairi kwa mnyororo ili kuzuia lisitembee hadi mdaiwa atakapolipa kiasi anachodaiwa.

 

Baadaye Wolper alipotoka na kukuta maofisa wa Tarura wamefunga gari lake, ndipo akaanzisha timbwili ambalo lilishuhudiwa na waandishi wetu ambao walinusa tukio na kufika.

 

“Huyu dada alifika hapa jana na kupaki gari lake, ilikuwa ni saa sita kamili, nikamuwekea tiketi ya shilingi 500 ya saa moja.

 

“Lakini cha kushangaza, aligoma kulipa, mimi sikutaka kujibizana naye kwa sababu alijifanya kujua sheria zaidi yangu.

“Nilichokifanya nilitoa taarifa ofisini, ndipo hawa mabosi wangu wakaja kudai ushuru wa jana ambao bado anaendelea kuugomea,” alisema mtoza ushuru wa Tarura ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake.

 

Hata hivyo, gomagoma ya Wolper ilikosa nguvu baada ya kuambiwa kuwa hiyo ni sheria na kwamba kwa kitendo alichokifanya jana yake, alitakiwa kupigwa na faini, jambo ambalo lilimfanya awe mpole.

 

Kufuatia hali hiyo, maofisa wa Tarura walimpatia elimu ya ushuru wa maegesho na kumsamehe kumpiga faini kwa vile aliwaahidi kuwa tangu siku hiyo atakuwa akilipa ushuru bila tatizo.

 

MASHUHUDA WANENA

Kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Majuto, alisema kuwa Wolper alikuwa na makosa, si kwa sababu ya kutokulipa kodi, bali kuzua ugomvi.

 

“Mimi kwa upande wangu naona Wolper naye ana makosa, maana hata kama mtu ni mgeni maeneo hayo, lazima uulizie utaratibu na si kugoma na kuanza kusababisha vurugu.

 

“Kama hujui sheria, unatakiwa uelekezwe na uelewe na si kuwa mgomvi.”

Kijana mwingine aliyejitaja kwa jina moja la Athumani alisema, maofisa wa Tarura wamekuwa kero kubwa kwa waendesha magari kutokana na kuwalipisha ushuru hata watu wanaopaki kando ya barabara kwa dakika chache.

 

“Mtu anaweza kuwa si mwenyeji wa eneo husika, sasa akipaki pengine aende kuuliza, haraka Tarura wanakuja kuweka tiketi ya kulipia 500.

“Ina maana madereva hawatakiwi kupaki hata kwa dharura za kutaka kuelekezwa jambo fulani.”

Hata hivyo, sheria ya Tarura inaelekeza kuwa maegesho yote hasa ya mijini yasiyo rasmi yanayomilikiwa na serikali, yanatakiwa kulipiwa ushuru wa shilingi 500 kwa sasa.
Toa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *