Kizimbani Hasara ya Mil 48 kwa TRA

Mtu mmoja amefikishwa mbele ya mahakama ya hakimu mkazi kisutu akikabiliwa na makosa manne ikiwemo ya uhujumu uchumi kwa kuisababishia hasara mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) ya shilingi milioni 48.

 

Geoffrey Kilimba, amesomewa mashitaka hayo mbele ya hakimu mkazi mfawidhi Godfrey kusaya na wakili wa serikali Mkuu, Paul kadushi, pamoja na wakili wa serikali mwandamizi, Wankyo Simon, ambapo wamedai kuwa upelezi wa Shauri hilo bado unaendelea.

 

Mshitakiwa anadaiwa kujihusisha na genge la uhalifu kati ya Agosti 29,2013 na Agosti 8,2020 akiwa na watu ambao hawapo mbele ya mahakama hiyo ambao walisaidia utendaji wa kosa la uhujumu uchumi.

 

Katika Shitaka la pili Kilimba anadaiwa kati ya Agosti 29,2013 na Agosti 8,2020 katika mkoa wa Dar es salaam, alitenda kosa la kukwepa kodi bila sababu ya msingi ikiwa ni zaidi ya shilingi milioni 48,806,922 ambayo ilipaswa kulipwa TRA.

 

Katika shitaka la tatu mshitakiwa kati ya Agosti 29,2013 na Agosti 8,2020 alisababishia hasara mamlaka ya mapato Tanzania kiasi cha shilingi milioni 48,806,922.

 

Katika shitaka la nne kati ya Agosti 29, 2013 na Agosti 8,2020 katika mkoa wa Dar es salaam alijipatia fedha milioni 48,806,922 huku akijua fedha hizo ni haramu.

 

Aidha Hakimu Isaya ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 30 ambapo amedai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na pia dhamana ya mshitakiwa imezuiliwa kisheria.

 Toa comment