Kocha Simba Ashtuka, Fasta Awabadilishia Mfumo Mtibwa

KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Sven Vandenbroeck, ameuangalia Uwanja wa Jamhuri wa mkoani Morogoro na fasta akachukua maamuzi ya kubadili mfumo wa uchezaji atakaoutumia kupiga mipira mirefu wakati timu yake itakapokuwa uwanjani leo ikicheza na Mtibwa Sugar.

 

Simba leo inatarajiwa kucheza mchezo wake wa pili wa ligi dhidi ya Mtibwa kwenye Uwanja wa Jamhuri hiyo ni baada ya kutoka kucheza na Ihefu FC kwenye Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya ambao ulimalizika kwa timu hiyo kushinda mabao 2-1.

 

Katika kuelekea mchezo huo, kikosi cha Simba huenda kikawa na mabadiliko machache baada ya wachezaji wake wanne kurejea kikosini baada ya kuukosa mchezo uliopita kutokana na matatizo ya kifamilia ambao ni Chris Mugalu, Luis Miquissone, Pascal Wawa na Gerson Fraga.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Sven alisema kuwa amelazimika kubadili mfumo wa uchezaji kutokana na sehemu ya kuchezea (pitch) sio nzuri tofauti na ile ya Uwanja wa Sokoine, hivyo haraka amewataka wachezaji kucheza kwa tahadhari.

 

Sven alisema kuwa, amegundua ubovu wa uwanja huo baada ya kufanya mazoezi kwa mara ya kwanza kwenye uwanja huo ambao hauna tofauti kubwa na ule wa Sokoine walioutumia mchezo na Ihefu wikiendi iliyopita.

 

Aliongeza kuwa katika kuelekea mchezo huo dhidi ya Mtibwa, amepanga kubadili mfumo kwa kuwataka kucheza pasi ndefu na siyo kupiga fupifupi ambapo hutumia zaidi wakiwa kwenye uwanja mzuri.

“Mchezo uliopita dhidi ya Ihefu mara nyingi ilibidi tutumie mipira mirefu kwa kuwa hatukuweza kucheza soka letu la pasi fupi fupi sababu ya uwanja kutokuwa mzuri.

 

“Nimeuangalia Uwanja wa Jamhuri ni mbovu haupo vizuri sehemu ya ‘pitch’ ambao hauna tofauti kubwa na ule wa Sokoine kidogo mzuri ambao kabla ya mchezo niliwataka kucheza mipira mirefu wakati tukiwa na mpira tukishambulia goli la wapinzani.

 

“Wachezaji wangu wapo kwenye hali nzuri tumefanya mazoezi kuangalia sehemu ya kuchezea sio nzuri lakini tumejipanga kukabiliana na hali yoyote tutakayokutana nayo,” alisema Sven.Toa comment