Kumekucha! Zitto, Mdee, Mnyika, Kubenea Upinzani Mkali 2020

17 0

Kumekucha! Zitto, Mdee, Mnyika, Kubenea Upinzani Mkali 2020

JOTO la uchaguzi ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), limeanza kupanda baada ya wagombea zaidi ya 72 kujitokeza kuwania ubunge katika majimbo 10 ya uchaguzi ya Jiji la Dar es Salaam.

 

Akizungumza na chombo kimojawapo cha habari nchini, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alisema chama hicho kimeshafunga pazia kwa watia nia wa ubunge na udiwani Machi 30, baada ya kufunguliwa tangu Januari 29, mwaka huu.

 

“Kwa mfano katika Mkoa wa Dar es Salaam katika majimbo 10 ya uchaguzi, kuna wagombea mbalimbali waliojitokeza zaidi ya 72, unaweza ukaona ni jinsi gani mwitikio umekuwa mkubwa, hakuna jimbo lenye wagombea chini ya watatu,” alisema Mrema.

 

WABUNGE MAARUFU WAPATA UPINZANI
Aidha, alisema kuwa Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe, amepata mpinzani ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Sabreena Sungura.

 

Mbunge wa Kibamba ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, amepata wapinzani wawili, ambao ni madiwani katika jimbo hilo.

 

Wengine ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), na Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, ambao wamepata wapinzani zaidi ya mmoja, ambao wanataka kuwania ubunge kwenye nafasi hizo.

 

Mdee amepata wapinzani wawili, mmojawapo akiwa ni mwanachama wa Chadema, Joel Mwakalebela.
Katika jimbo la Ubungo, wamejitokeza watia nia sita akiwamo Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob, kuchuana na Kubenea.

 

Hata hivyo, baadhi ya wabunge hawakutia nia ya kugombea nafasi mbalimbali ambao ni Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, Mbunge wa Moshi Mjini, Jaffar Michael, Mbunge wa Moshi Vijijini, Anthony Komu na Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare.

 

Katika mchakato huo, wapo wabunge wanaotarajia kubadili majimbo ya kugombea, ambao ni Mbunge wa Momba, David Silinde, aliyetia nia katika jimbo la Tunduma ambalo kwa sasa linaongozwa na Frank Mwakajoka.

 

Katika Jimbo la Kinondoni, wamejitokeza watu wanne akiwamo Mbunge wa Viti Maalum, Suzan Lyimo na Diwani wa Kinondoni, Mustapha Muro, huku jimbo la Segerea wakijitokeza wagombea wanne, akiwamo Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema na madiwani wawili Patrick Asenga na Manase Mjema.

 

Baadhi ya viongozi walio katika nyadhifa mbalimbali katika chama hicho waliojitokeza kugombea katika majimbo ni Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Victoria, Ezekiel Wenje, anayegombea jimbo la Nyamagana, Mwenyekiti wa Kanda ya Kusini, Selemani Mathew, anayegombea jimbo la Mtama, Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Grace Tendega, anayegombea jimbo la Kalenga
Wengine ni Patrick Sosopi (Isimani) ,Sophia Mwakagenda (Rungwe), Catherine Ruge (Serengeti), Joyce Sokombi (Musoma Mjini), Salome Makamba (Shinyanga Mjini), Grace Kiwelu (Vunjo), Hemed Ali (Lindi Mjini), Yoseph Komba (Muheza), Tunza Malapo (Mtwara Mjini), Rebecca Mdogo (Arumeru Mashariki), Lucy Owenya (Moshi Vijijini) na Gimbi Masaba (Musoma Mjini).

 

Kwa pande wa nafasi ya urais, Mkurugenzi huyo wa Chadema, alisema hawajafungua milango, lakini kanuni zinaruhusu yeyote mwenye nia ya kugombea kiti hicho kumwandikia barua Katibu Mkuu wa chama hicho kuhusu nia yake.
Toa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *