Kusajili Drone Dola 100 kwa Mwaka, Hizi Zinaweza Kuwa Silaha

Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania SACP David Misime, amesema kuwa Ndege zisizokuwa na Rubani maarufu kama drone, zisiposajiliwa zinaweza kutumia kwa nia ovu ili kuihujumu nchi huku pia ikielezwa kuwa Zinaweza kutumika kama silaha na kuleta maafa kwa Taifa.

 

Taarifa hiyo imetolewa hii jana Agosti 31, 2020, ambapo katika kutekeleza hilo Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Tanzania na Jeshi la Polisi kwa pamoja wameamua kushirikiana na kuunda kikosi kimoja, ambacho kitaweza kusimamia utekelezaji wa kanuni ambayo inawataka wamiliki wote wa Drones kuzisajili.

 

“Drone zinaweza kutumika kuihujumu nchi kwa kuchukua taarifa kwa nia ovu, hivyo ukikamatwa unaiendesha bila kibali ni kosa la jinai kama yalivyo makosa mengine. Tupo katika ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia, lakini teknolojia nyingine lazima tuhakikishe tunadhibiti madhara yanayoweza kujitokeza mbeleni na hii ni kwa faida ya Watanzania wote,” amesema Msemaji wa Jeshi la Polisi.

 

Awali akizungumza, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA), Hamza Johari amesema kuwa, usajili wa drone ni Dola 100 kwa kila mwaka na haitumiki nchi nzima;

 

“Ndege Nyuki (drones) sio Camera za kawaida, inaweza kugeuka silaha na ikaleta maafa kwa Taifa, hivyo baada ya kuisajili ili itumike lazima uwasiliane na Ofisi ya Serikali ya Mtaa husika pamoja na Jeshi la Polisi. Ukibainika unatumia Drone bila kusajili, adhabu yake ni Shilingi Milioni moja au kwenda jela miezi sita.

 

“Usajili wa Drone ni dola 100 ambayo utalipa kila mwaka, hakuna kibali cha kurusha Drone nchi nzima ni kila mkoa, hivyo kama umesajiliwa Dar es Salaam ukihitaji kwenda mkoa mwingine kikazi utakuja kuomba kibali tena. 

 

Mbali na hayo imeelezwa kuwa ikibainika mtu anatumia drone bila kusajili, adhabu yake ni faini ya Shilingi Milioni Moja au kifungo cha miezi sita jela.Toa comment