Lissu Ashindwa Tena Kufika Kortini, Sababu Hii Hapa!

3 0Lissu Ashindwa Tena Kufika Kortini, Sababu Hii Hapa!

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo  (CHADEMA), Tundu Lissu, ameshindwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar ambapo anakabiliwa na kesi ya uchochezi.

 

Lissu ambaye ilikuwa afike mahakamani hapo mapema leo Jumatano, Agosti 25, 2020, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Kassian Matembele, ameshindwa kufika kwa sababu ya kukwamishwa na mchakato wa kurudisha fomu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) uliomalizika jana usiku.

 

Wakili wa Lissu, Peter Kibatala, amesema kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na NEC, Lissu na mgombea mwenza wake walitakiwa kurudisha fomu za kugombea urais na kupatiwa za uteuzi majira ya saa sita mchana kisha aanze safari za kurejea jijini Dar es Salaam kuhudhuria kesi zake.

 

“Bahati mbaya mpaka saa 2:30 usiku wagombea hao walikuwa hawajatoka katika ofisi za tume, hivyo kusababisha ratiba zake za usafiri kurejea Dar es Salaam kuharibika. Naiomba mahakama iridhie kuahirisha kesi hii ipangwe siku nyingine ambayo naamini mshtakiwa atakuwepo mahakamani,” amesema Kibatala.

 

Baada ya Kibatala kueleza hayo, Wakili wa Serikali Mkuu, Renatus Mkude, amedai kuwa kwa mazingira hayo yaliyoelezwa na Wakili wa Utetezi hawana pingamizi, hivyo rai yao shauri hilo liahirishwe hadi tarehe nyingine inakubalika. Hakimu Mkazi Mwandamizi Kassian Matembele ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 24, mwaka huu.

 

Katika kesi hiyo namba 123 ya mwaka 2017, Lissu anadaiwa kutoa maeneno ya uchochezi wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Deman, Zanzibar, Januari 11, 2017, akiwa eneo la Kibunju Maungani, Wilaya ya Magharibi B, mkoni Mjini Magharibi.

 

Inadaiwa siku hiyo Lissu alisema maneno: “Tangu mwaka 1964 Tanganyika ndiyo inayoamua nani atawale Zanzibar… Tangu mwaka 1964 Zanzibar inakaliwa kijeshi na Tanganyika, nani anayebisha… Tangu mwaka 1995 ikifika uchaguzi askari wa Tanganyika wanahamia Zanzibar ili kuja kuhakikisha kuwa vibaraka wao wa Zanzibar hawaondoki na wananchi wa Zanzibar mnapigwa, mnateswa, mnauawa, kwa sababu ya ukoloni wa Tanganyika kwa Zanzibar.”

 

Pia, anadaiwa katika tarehe hiyo Lissu alitamka kuwa; “Marehemu Karume alipoanza kushtuka mwaka 71, 72 akauawa…, itakapofika tarehe 15 mwezi wa kwanza mnaadhimisha miaka 53 ya kukaliwa kijeshi na Tanganyika.”

 

”Jumbe aliondolewa Dodoma na Ally Hassan Mwinyi alipewa urais wa Zanzibar Dodoma, aliyempa ni Nyerere na si Wazanzibar… Marais wa Zanzibar wote ni made in Tanganyika..”

 

“Zanzibar wanatawaliwa na Tanganyika kwa kivuli cha Tanzania, Tanzania ni Tanganyika …, Tanganyika ni kivuli tu cha kuikalia Zanzibar, cha kuigeuza Zanzibar koloni na makoloni huwa yanawanyanyasa yanaowanyonya kisiasa, kiuchumi na kuyakandamiza kijeshi…

 

“Mmetawaliwa na Tanganyika kisiasa, miaka yote hii… Mohamed Shein hana lolote ni kibaraka tu siku watawala wakisema hatufai ataondolewa tu kama alivyoondolewa Aboud Jumbe.”Toa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *