Maeneo 5 Hatari kwa Corona Bongo Yaanikwa

27 0

Maeneo 5 Hatari kwa Corona Bongo Yaanikwa

WAKATI nchi mbalimbali duniani zikiimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 unaonezwa na virusi vya Corona, RISASI Jumamosi linakuchambulia maeneo matano hatari ambayo kila mtu anapaswa kuzidisha umakini ili asiambukizwe virusi hivyo hatari.

 

Virusi vya Corona ni hatari duniani kwa sababu takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha hadi kufikia Machi 26, mwaka huu watu 475, 890 wameambukizwa, 21, 367 wamefariki wakati waliopona ni 114, 822.

 

Aidha, Tanzania takwimu zinaonesha walioambukizwa ni 13, hakuna kifo lakini aliyepona ni mmoja pekee. Watu wawili waligundulika Arusha vivyo hivyo Zanzibar, Kagera mmoja na Dar es Salaam nane.

 

Ili kujikinga na ugonjwa huo, maeneo yenye mikusanyiko mingi ya watu kama vile maeneo ya sokoni, vituo vya mabasi/daladala (stendi), madanguro, baa na maeneo ya miji ni baadhi ya maeneo hatarishi kwa virusi hivyo.

 

MAENEO YA SOKONI

Mikusanyo katika maeneo ya sokoni kama vile, Kariakoo, Mabibo kwa upande wa Jiji la Dar ni moja ya maeneo hatari kwa maambukizi ya virusi vya Corona.

 

Timu yetu ya waandishi imetembelea maeneo hayo na kushuhudia wananchi wakinunua bidhaa mbalimbali katika masoko hayo, na kuchangamana bila kuchukua tahadhari yoyote.

 

“Mazingira ya soko hili la Mabibo si rafiki kiafya kwa binadamu kwa sababu miundombinu ni mibovu hali ambayo huwezi kuzingatia suala la usafi katika eneo hili,” alisema Mariam Sadick mfanyabiashara katika eneo hilo.

 

VITUONI

Katika maeneo ya vituo vya daladala RISASI limebaini kuwa hakuna utekelezaji wowote wa agizo la Serikali kuhusu daladala kupakia abiria ‘levo siti’.

 

Pamoja na hilo, vilevile katika vituo vingi hakuna tahadhari yoyote inayochukuliwa na abiria hata mamlaka husika zinazosimamia vituo hivyo.

 

MAENEO YA BAA

Baadhi ya wamiliki wa baa wamefuata maelekezo ya Serikali kuweka maji na sabuni au vitakasa mikono, hata hivyo uwepo wa huduma hizo za baa bado ni hatari kwa maambukizi ya virusi hivyo kwa sababu wateja wa baa hizo wakishakunywa pombe na kulewa husahau kuchukua tahadhari.

 

“Mtu akiingia ananawa mikono, akianza kunywa ya kwanza ya pili wala hakushiki wakati mnazungumza, ila zikikolea, ataanza kukushika kama rafiki mwenzie mnayepiga naye stori na hapo ndipo hatari inaweza kutokea kwa sababu huwezi kujua kama alikohoa akaziba kwa viganja au chochote,” alisema mmoja wa wateja wa baa ya Facebook, Sinza.

 

MADANGURO

Licha ya baa kuwa eneo mahususi kwa machangudoa kujitafutia wateja, vilevile katika madanguro ambayo hufanyia ufuska huo bado ni eneo hatari kwa kusambaza virusi hivyo.

 

MAENEO YA MIJI

Mkusanyiko mkubwa watu ndio tatizo au chanzo kikuu cha kusambaa kwa virusi hivi, ndio maana nchi nyingi zilizozidiwa na Corona huamuru wananchi wake kusalia ndani kwa muda fulani.

 

Hata takwimu zinaonesha Jiji la Dar ndilo linaloongoza Tanzania kwa kuwa na wagonjwa wengi (8) kwa sababu tu ya uwingi wa watu ambao hadi sasa inakadiriwa wamefikia milioni tano.

 

Kwa maana hiyo maeneo ya miji kama vile Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na miji mingine yenye mikusanyiko mikubwa ya watu bado ni hatari hivyo wananchi wanapaswa kuzidisha umakini.

 
Toa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *