Malaika; Mwana Mpotevu Amerudi! – Global Publishers

10 0Malaika; Mwana Mpotevu Amerudi!

Diana Exavery almaarufu Malaika, ni mwanamuziki mwenye kipaji cha kipekee kwenye Bongo Fleva. Mwaka 2013, ndipo Chege alisikia sauti yake, akaamua kumshirikisha kwenye Ngoma ya Uswazi Take Away.

 

Baada ya hapo, ameendelea kuachia ngoma zake mwenyewe, ikiwemo Mwantumu, Nenda Pamoja, Rarua, Zogo na Saresare aliyomshirikisha Producer Mensen Selekta wa Studio za De Fatality Music.

 

Malaika ni miongoni mwa wanamuziki wa kike wasioshikika kwenye Bongo Fleva, japokuwa hapo katikati alipotea kidogo, lakini sasa amerudi na kuzidi kuwaonesha mashabiki wake kipaji alichonacho.

 

Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, limemvuta Malaika kwenye mahojiano maalum (exclusive interview), ambapo kubwa zaidi ni kuvunja ukimya wake kwa kuachia ngoma kali, ambayo iko mtaani kwa sasa.

IJUMAA WIKIENDA: Mashabiki wangependa kujua, Malaika alijificha wapi kwa kipindi kirefu bila kuachia kazi mpya?

MALAIKA: Kila mtu anapofanya kazi, kuna mikakati anajiwekea ili kazi zake zizidi kuwa na ubora. Kukaa kimya ni moja ya mipango na changamoto za hapa na pale.

IJUMAA WIKIENDA: Je, mashabiki wamekupokea vipi baada ya ukimya?

MALAIKA: Mapokezi yamekuwa mazuri na hata nilivyotoa ngoma yangu ya Baila, ilikuwa inanipa hofu, maana wasanii wengi wanaopotea, wakirudi huwa wanapwaya.

IJUMAA WIKIENDA: Tunajua Uswazi Take Away ndiyo ngoma iliyokutambulisha, je, baada ya hapo ilikupa mianya gani kwenye muziki?

MALAIKA: Uswazi ilinifungulia njia kwa sababu nilifanya na msanii mkubwa ambaye ni Chege, hivyo nikaanza kujulikana zaidi na kufungua njia ya kazi zangu mwenyewe.

IJUMAA WIKIENDA: Unamzungumziaje Chege kama mtu aliyekutambulisha kwenye gemu?

MALAIKA: Chege ni kaka yangu na ninaweza kumuita baba yangu kwenye muziki, chochote ninachokifanya kuhusiana na muziki, huwa ninamshirikisha na ananisapoti sana. Hata wakati nipo kimya, alikuwa akiniuliza kama kuna shida.

IJUMAA WIKIENDA: Umetambulika na Ngoma ya Uswazi Take Away na mpaka kutoa kazi nyingine, unaona ushirikiano gani kwa mashabiki wako?

MALAIKA: Tangu nimeanza, naona watu wamenipokea vizuri mpaka sasa na wanaendelea kunipokea.

IJUMAA WIKIENDA: Je, kwa mtu anayefuatilia kazi zako, atazipata vipi?

MALAIKA: Wakati ninaanza, sikuwa na Chaneli ya YouTube, ila nilipotoa kazi yangu mpya, imepata karibu wafuasi elfu tisa na si kitu cha kawaida kwa mtu ambaye anaanza kumiliki chaneli.

IJUMAA WIKIENDA: Umekuwa slow kwenye kutoa kazi, je, ni staili yako au?

MALAIKA: Ni changamoto za wasanii wa kike katika kuhakikisha anafanya kazi nzuri na kupanda kila siku, huwa nathamini sana kutoa kazi nzuri kwa mashabiki wangu.

IJUMAA WIKIENDA: Unaionaje tasnia ya muziki baada ya kurudi kwenye gemu, hasa kwa wasanii wa kike?

MALAIKA: Gemu limebadilika, maana nimekaa kama miaka minne kimya, ila nimerudi naona mabadiliko. Maana wasanii wa kike wamekuwa wengi.

IJUMAA WIKIENDA: Ulikuwa nje ya gemu kwa muda mrefu, je, unakubalika kama mwanzo?

MALAIKA: Bado nipo kwenye ‘status’ yangu. Hata nilipokuwa kimya, mashabiki walikuwa wakiuliza niko wapi, wakitaka nirudi.

IJUMAA WIKIENDA: Mipango yako iko vipi, maana kila kukicha zinaibuka kazi mpya za wasanii wengine?

MALAIKA: Mipango na mikakati ni kufanya kazi nyingi ambazo zitawafikia mashabiki wangu popote walipo.

IJUMAA WIKIENDA: Hujaonekana kufanya kazi na wasanii wa kike, je, shida ni nini?

MALAIKA: Kama timu yangu, tuna imani ya kufanya kazi nyingi tu na wasanii wa kike.

IJUMAA WIKIENDA: Uliwahi kuonekana kwenye filamu pia, lakini baadaye ukapotea, kitu gani kilitokea?

MALAIKA: Siendelei kucheza filamu, maana niliitwa kwa heshima ya Mzee Kambi, alikuja kuniomba kutokana na uhusika tu. Ndoto yangu kubwa ni kwenye muziki na si filamu na ndiyo maana bado naendelea kuachia ngoma tu.

IJUMAA WIKIENDA: Tukirudi kwenye maisha yako binafsi, umekuwa mkimya sana kwenye uhusiano wako, je, ndiyo aina ya maisha uliyochagua kuishi?

MALAIKA: Unajua nipo kwa ajili ya kuwapa mashabiki muziki mzuri na si mambo yangu binafsi.

IJUMAA WIKIENDA: Wewe ni mwanamke mzuri na pia maarufu, je, unapitia usumbufu wowote?

MALAIKA: Usumbufu upo kwa mwanamke yeyote, ishu ni kujitambua tu na mimi niko kwenye uhusiano.

IJUMAA WIKIENDA: Mipango ya ndoa imekaa vipi kwa upande wako?

MALAIKA: Ndoa ni kitu cha heri na huwa kinatokea kwa mtu yeyote.

IJUMAA WIKIENDA: Umerudi na utofauti hasa kwenye urembo wako, nini kilikusukuma kufanya teeth braces (urembo wa meno)?

MALAIKA: Hii ilikuwa ni kiu yangu kutengeneza urembo wa meno ili kupata tabasamu zuri na mpangilio mzuri wa meno.

IJUMAA WIKIENDA: Je, haupitii changamoto yoyote? MALAIKA: Changamoto kubwa ni watu wanakuwa wananishangaa, ila mimi naona kama ni kawaida.

IJUMAA WIKIENDA: Marekebisho hayo yamekugharimu kiasi gani cha pesa?

MALAIKA: Imenigharimu kiasi cha shilingi milioni nne za Kitanzania na hii ni bei ndogo tu kwa hapa kwetu, ila nchi za wenzetu wanazingatia sana.

IJUMAA WIKIENDA: Muziki wako mpaka sasa unaona umekulipa?

MALAIKA: Mara nyingi sipendi kutaja mafanikio, japokuwa yapo mengi maana sitaki kuwaharakisha vijana hasa waliopo shuleni, wakaacha masomo wakiamini huku kuna mafanikio makubwa.

Makala: Happyness Masunga, Bongo.

 Toa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *