Mambo 5 Yanga Inatakiwa Kuyafanya Ili Kuwalipa Mashabiki

10 0Mambo 5 Yanga Inatakiwa Kuyafanya Ili Kuwalipa Mashabiki

HATIMAYE pilikapilika za usajili wa wachezaji kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, zimefikia tamati juzi saa 5:59 usiku baada ya kila timu kuongeza wachezaji wake iliowakusudia kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Bara unaotarajia kuanza kutimua vumbi Septemba sita.

 

Dirisha la usajili la wachezaji wa ligi kuu, linatarajiwa kufungwa rasmi juzi usiku Agosti 31. Awali lilifunguliwa Agosti Mosi. Mabingwa wa kihistoria Yanga wenyewe wamefanya usajili wa wachezaji tisa kuelekea msimu ujao huku ikiwatema nyota kadhaa waliokuwa tegemeo katika kikosi hicho akiwemo beki Kelvin Yondani na Juma Abdul.

 

Yanga imesajili wachezaji nyota wakiwemo Tuisila Kisinda na Mukoko Tonombe kutoka AS Vital ya DR Congo ambao ni miongoni mwa wachezaji waliopokelewa kwa kishindo cha hali ya juu kutoka kwa mashabiki wao ambao wamekuwa na matumaini makubwa kutoka kwao kuelekea msimu ujao wa ligi kuu.

 

Mabingwa hao wa kihistoria wapo katika mchakato wa kuhakikisha wanafanikiwa kutwaa ubingwa msimu ujao kutokana na kuukosa kwa misimu mitatu mfululizo ambayo ni 2017/18, 2018/19 na 2019/20, jambo ambalo liliwanyima furaha mashabiki wa timu hiyo kutokana na kukosa mataji hayo.

 

Hivyo basi, usajili walioufanya hivi sasa kuelekea msimu ujao, umewavuta mashabiki wa timu hiyo ambao wanahitaji kuiona timu yao inarudi katika kiwango chake kile cha misimu mitatu nyuma kwani wamechoka kuona kombe linaelekea Msimbazi ‘kila kukicha’.

 

Hivyo wamekuwa na matumaini mapya kutokana na usajili uliofanyika hivi sasa. Championi linakuchambulia mambo ambayo Yanga wanatakiwa kuyafanya ili kulipa fadhila kwa mashabiki wao kuelekea msimu ujao wa ligi kuu kutokana na muitikio walioufanya katika kuwapokea wachezaji.

 

MATOKEO MAZURI KWENYE LIGI

Piga ua, Yanga inahitaji kupata matokeo mazuri katika mechi zake za ligi kwa kupata pointi tatu na kujiwekea mazingira mazuri ya ushindi na iwapo itatokea watapoteza mechi hawataeleweka.

 

Msimu uliopita Yanga katika mechi zake 38 ilizocheza, iliweza kushinda mechi 19 tu huku ikitoa sare michezo 15 na kupoteza michezo minne, hivyo hali hiyo iliwanyima ubingwa ambapo watani wao Simba walimaliza ligi kwa kushinda michezo 27, sare saba na kupoteza michezo minne kati ya 38 iliyocheza, hivyo wanahitaji kubadilika msimu ujao kwa kufanya vyema ili kuleta furaha kwa mashabiki.

 

WACHEZAJI KUONYESHA VIWANGO

Wachezaji waliosajiliwa watambue kuwa wana deni kubwa kuelekea msimu ujao wa ligi kuu kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika kila mechi ili kuendana na thamani ya usajili wao na mapokezi waliyopewa na mashabiki wa timu yao.

 

KUTWAA UBINGWA WA LIGI

Ni misimu mitatu sasa mfululizo Yanga haijatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kuanzia msimu wa 2017/18, 2018/19 na ulioisha hivi karibuni wa 2019/20 ambapo mashabiki wamekuwa na hamu kubwa ya kufanikiwa kutwaa ubingwa huo katika msimu ujao.

 

Hali inaonyesha wazi iwapo watashindwa kutwaa ubingwa msimu ujao, basi kuna hatari mbeleni, mashabiki kutowaelewa viongozi na wanaweza wakahoji kama wanastahili kuendelea kuitumikia klabu hiyo tena.

 

KOMBE LA SHIRIKISHO

Yanga inahitaji kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC), maarufu kama Kombe la FA msimu huu baada ya kulikosa misimu miwili mfululizo wa 2018/19 na 2019/20, hivyo wana deni kubwa kuhakikisha wanafanikiwa kulitwaa kombe hilo ambalo lipo mikononi mwa watani wao Simba ambao walilitwaa baada ya kuwafunga Namungo.

 

UTAWALA BORA

Viongozi chini ya mwenyekiti Dk Mshindo Msolla, wanatakiwa kusimamia majukumu yao kikamilifu kuhakikisha Klabu ya Yanga haitetereki kuelekea msimu ujao wa ligi kuu kwa kuhakikisha wachezaji wanapatiwa mahitaji yao yote kwa wakati ili kuweza kutekeleza majukumu yao.

 KHADIJA MNGWAI, Dar es SalaamToa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *