Meridianbet yamwaga misaada Ocean Road Hospital


KAMPUNI ya Michezo ya Bahati Nasibu ya Meridianbet kwa kushirikiana na taasisi ya Lions Club ya Dar na Pwani, imetoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya milioni moja kwa wagonjwa wa saratani katika Hospitali Kuu ya Saratani ya Ocean Road, Dar.

Gavana wa Lion Club Tanzania, Bakari Omary amesema msaada huo ni sehemu ya faraja inayotolewa na taasisi hiyo katika kuadhimisha siku ya saratani duniani ambayo huadhimishwa kila Septemba.

Omary amesema kuwa msaada wanaotoa ni kwa lengo la kurejesha kwa jamii pamoja na kuwatia moyo wagonjwa na kuwapa matumani watambue kuwa jamii inayowazunguka inawathamini na kuwajali.

Mtendaji Mkuu wa Meridian Bet , Carlo Njato, amesema wameamua kuifadhili taasisi hiyo ili kuongeza nguvu ya kuwasaidia wagonjwa wa saratani ambapo matibabu yake ni gharama ukilinganisha na kipato cha walio wengi.

Naye Muuguzi Mkuu wa Ocean Road, Jesca Kawegele amewapongeza watoaji wa msaada huo na kuiomba jamii kuwa na utamaduni wa kuwasadia wagonjwa wa saratani hususani wale wa Ocean Road ambayo ndiyo inayopokea wagonjwa wengi nchini.

“Wahitaji ni wengi kutokana na ukubwa wa tatizo. Wanakaa sana wodini hivyo wanahitaji kusaidiwa na jamii. Serikali ya Tanzania inajitahidi kuwahudumia kwa kiasi chake, lakini bado kuna changamoto za uhitaji kulingana na wingi wa wagonjwa,” amesema.

Msaada huo ni pamoja na matunda, miswaki na dawa za meno, sabuni za kufulia na kuogea, sanitary pad, mafuta ya kupaka, vifaa vya usafi na gloves.
Toa comment