Mgogoro na Mkewe… Mume Ajichongea Jeneza

29 0

Mgogoro na Mkewe… Mume Ajichongea Jeneza

CHANZO ni kuwa na mgogoro na mkewe, Sylvester Mihayo (45) amefikia uamuzi mgumu wa kujichongea jeneza ili siku akifa mambo yasiwe mengi atakapozikwa, Risasi linakusogezea habari hii ya kipekee.

 

Mbali na kutoelewana na mwandani wake aliyezaa naye watoto nane, Mihayo ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Butambala Kata ya Igulwa, Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita, amesema anakiona kifo chake kwa kile alichokitaja kuwa ni kuugua kwa muda mrefu magonjwa ya ajabu yasiyokuwa na tiba.

 

MSIKIE MIHAYO

Machi 24, mwaka huu alipozungumza na mwandishi wetu, Mihayo alidai kuwa chanzo cha yote anayopitia ni mkewe aliyemtaja kwa jina la Vumilia John.

 

“Ndugu yangu mwandishi wa habari, mimi kujichongea jeneza siyo kwamba nitajidhuru, bali nimejitabiria kufa.

“Kutokana na haya ninayopitia ndani ya familia yangu, ndiyo maana nimeona nichonge jeneza hili ili mauti yakinikuta, litumike kunizika.”

 

Aidha, weledi wa kihabari unakwaza kufunua wazi yale aliyoyaita mapito ndani ya familia yake, kwa sababu mengi yamejaa imani za kishirikina.

Hata hivyo, Mihayo anaeleza kwa masikitiko kuwa, kwa muda wa miaka mitatu, amekuwa akiumwa ugonjwa ambao hauonekani kwenye vipimo vya kitabibu na wala hautibiki.

 

KISHEREHESHI CHA MGOGORO

Katika hatua nyingine, mwanaume huyo alisema pamoja na kusumbuliwa na ugonjwa kwa muda mrefu, familia yake kwa maana ya mke na watoto wake, wamemtelekeza.

Anaeleza kuwa mkewe Vumilia, amekuwa akisapotiwa na watoto wao katika kumfanyia kile alichotaja kuwa matendo ya ukatili.

 

Isitoshe alidai kwamba kwa sasa mke wake amegeukia kazi ya uganga wa kienyeji na kwamba hadi sasa anaishi na watoto wake katika eneo lingine alilojenga nyumba.

“Kwa sasa familia yangu, wamejenga nyumba nyingine eneo la Maghorofani Ushirombo ili waendeshe uganga wao kwa uhuru, mimi wameniacha nateseka hapa.

 

“Ndugu yangu, tangu mwaka 2018 nimeteswa na ugonjwa huu usiojulikana hadi leo sijapata nafuu.

“Hospitali nyingi nimekwenda, wakinipima hawaoni ugonjwa, lakini mimi najisikia naumwa sana. Nimekwenda kwa waganga wa kila aina wa kienyeji, lakini bado sijapona,” alisema Mihayo.

 

ABUBUJIKWA MACHOZI

Katika hali ya kuonesha kuwa na uchungu mwingi moyoni mwake kuhusu anayopitia, Mihayo alimwaga machozi mbele ya mwandishi wetu na kusema: “Hata hapo nilipokuwa naishi, nimekimbia. Nakaa kwenye karakana yangu ya kuchomelea vyuma.”

 

Kwa nini amekimbia makazi yake aliyoachiwa na mkewe? Mihayo anasema tena: “Naogopa kumalizwa.”

Ingawa alitaja waziwazi kitakachommaliza, lakini maadili yanazingatiwa kwa sababu mengi ni mambo ya kufikirika yasiyokuwa na uhalisia wa kitaaluma.

MIHAYO ADAI KUSIKIA SAUTI YA KUTOLEWA KAFARA

“Kuna wakati nilisikia watu (aliwataja kwa majina, lakini taaluma inazingatiwa) wakisema nitolewe kafara ili mambo yao yaende vizuri,” alisema Mihayo.

 

Aliongeza kwa kumuomba mwandishi wetu amsaidie kuweka mambo sawa ikiwa pamoja na kumpatanisha na familia yake.

“Nisaidie niwe karibu na familia yangu hasa watoto ili nife nikiwa chini ya mikono salama na waweze kusitiri mwili wangu, nisife kama mnyama,” alisema Mihayo kisha kuangua kilio.

 

Baada ya kunyamaza, mwanaume huyo ambaye jeneza alilolichonga, amelihifadhi chumbani kwa mama yake akisubiri kifo chake, aliendelea kueleza kuwa:

“Mimi sina shida na msaada wa kifedha, bado nina nguvu ya kutafuta na ninakula kila nitakachokihitaji, bali kikubwa ninachoomba ni serikali initatulie changamoto hizi zinazonikabili.

 

MZAZI WAKE AMWAGA MACHOZI

Mama mzazi wa mwanaume huyo; Veronika Kasase (86) mkazi wa kijiji cha Mwalo Kata ya Businda Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani hapa, akizungumza na mwandishi wetu nyumbani kwake huku akimwaga machozi wakati akisimulia mkasa wa mwanaye alisema:

 

“Mwanangu ametumia fedha nyingi sana kujitibia, lakini hajapona. Sijui hata nini kinamsumbua mtoto wangu jamani.

“Ameshatolewa maji tumboni na kukatwa nyama kwenye mbavu akapimwa kansa, lakini haikuonekana.

 

“Baada ya kuona haponi, ikabidi achonge jeneza lake na kulileta hapa kwangu kulihifadhi.

“Niliumia sana, nikawaita pamoja ili nijue kwa nini familia yao imesambaratika lakini mkwe wangu (Vumilia) alikataa.

“Yote nimemwachia Mungu, maana sina la kufanya zaidi ya kubaki nalia tu kama hivi kuhusu hali ya mwanangu,” alisema mama huyo.

 

VUMILIA ATAFUTWA

Mwandishi wetu alipomtafuta Vumilia kwa njia ya simu, alipokea na kusema:

“Siwezi kuzungumzia hilo, mimi niko Kahama kwanza nina mgonjwa.”

 

HUYU HAPA MKUU WA WILAYA

Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Said Nkumba alimwambia mwandishi wetu kuwa hajapata kisa hicho cha mtu kujitengenezea jeneza.

 

“Suala la kujiandalia jeneza siyo jambo la kushangaza sana ama kuleta taharuki kwa jamii, ila kama kuna changamoto nyingine kuhusu huyu bwana nitazifuatilia ili kuzitatua kwa sababu nimeletwa hapa kutatua changamoto za watu.”

STORI: MWANDISHI WETU, DAR
Toa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *