Mgombea Ubunge Avamiwa, Aporwa Fomu

MGOMBEA ubunge wa Morogoro Mjini kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Abeid Mlapakolo, amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro kwa kufanikisha kupatikana kwa fomu zake za kugombea ubunge wa jimbo hilo zilizokuwa zimeporwa na watu wasiojulikana.

 

Mlapakolo alisema tukio la kuvamiwa na kuporwa fomu hizo lilitokea jana asubuhi wakati akienda kwenye ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo kutekeleza matakwa ya sheria za uchaguzi kurejesha fomu kabla ya saa 10.

 

Alidai kuwa, akiwa nje ya jengo la ofisi ya msimamizi wa uchaguzi, ghafla kulitokea kundi la watu waliomvamia na kuanza kumshambulia kwa kumpiga sehemu mbalimbali za mwili kisha kumpora fomu na kutokomea nazo.

 

“Nilifika kurejesha fomu kama sheria inavyotaka kila mgombea arejeshe fomu kabla ya saa 10 jioni, lakini nikiwa nje, likaja kundi la watu kunivamia na kunipiga, wengine wakataka kunivunja mkono na fomu zangu wakakimbia nazo.

 

“Ninamshukuru Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, nilipompigia simu alinisaidia wale watu walikamatwa na fomu zangu zikarudi,” alisema Mlapakolo.

 

Aliliomba jeshi hilo kuimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali kuelekea uchaguzi mkuu kufuatia vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyoendelea hasa kuvamiwa kwa baadhi ya wagombea wa upinzani.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo watuhumiwa wa tukio hilo wameshakamatwa na wanaendelea kuhojiwa.

 

Aliwataka wananchama wa chama hicho kuwa watulivu wakati hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa na kwamba uchunguzi utakapokamilika, watuhumiwa watafikishwa mahakamani.Toa comment