Mke Ayabeba Mabao ya Morrison

KIUNGO Mshambuliaji wa Yanga, Bernard Morrison, amefunguka kuwa mabao yake yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na dua maalum ambazo zinafanywa na mke wake.

 

Morrison ameweka wazi kwamba mkewe anahusika kwenye mabao anayoyafunga kutokana na dua maalum ambazo anazifanya katika viatu anavyovivaa vikiwemo alivyomtungua kipa wa Simba, Aishi Manula kwenye dabi Machi 8, mwaka huu Yanga ikishinda 1-0.

 

Morrison tangu atue Yanga kwenye usajili wa dirisha dogo msimu huu, amehusika katika mabao sita ya timu hiyo akifunga matatu na kutoa asisti tatu.

Kiungo huyo ambaye hivi karibuni alisaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuichezea Yanga, amesema kufanya kwake vizuri uwanjani kunatokana na maombi ya mke wake pamoja na mwanae.

 

“Mke wangu na binti yangu wamekuwa na kawaida ya kuvifanyia sala viatu ambavyo nimekuwa nikivivaa, hiyo ndiyo sababu ya kufanya vizuri uwanjani.

 

“Hata walipokuja Dar kabla ya mechi na Simba waliniletea viatu ambavyo walivifanyia sala na hivyohivyo ndivyo ambavyo vikanifanya nifunge kwenye mechi hiyo ya watani.

 

“Awali nilipokuja hapa nilikuwa nina kiatu kimoja tu na ndiyo hichohicho nikakivaa kwa karibu mwezi mmoja kabla ya kuja kubadilisha baada ya kuletewa vingine na mke wangu,” alisema Morrison.
Toa comment