Morrison Alizua Yanga, Amenikera Kocha

27 0

Morrison Alizua Yanga, Amenikera Kocha

 

KOCHA Mkuu wa Klabu ya Yanga, Mbelgiji, Luc Eymael, amefichua kuwa, amekerwa na kitendo cha winga wa kikosi hicho, Mghana, Bernard Morrison, baada ya mchezaji huyo kumdanganya kocha wakati akiwa ameshakubali kusafiri naye jana.

 

Eymael alikuwa anajua kuwa jana asubuhi alipaswa kusafiri na David Molinga pamoja Morrison kuelekea mkoani Shinyanga kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mwadui utakaopigwa leo.

 

Lakini baada ya kufika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akajikuta akisafiri na Molinga huku akiwa hajui kwa sababu gani Morrison alishindwa kufika kwa ajili ya safari hiyo.

Eymael aliliambia Championi Jumamosi kuwa, Morrison hatakuwepo katika mechi ya leo dhidi ya Mwadui kwa sababu hajasafiri naye na amemkera kwa kuwa alimuahidi jana (juzi) asubuhi kuwa wangesafiri wote.

 

Eymael aliongeza kuwa, alimtumia tiketi na mara ya mwisho alimpigia simu mara mbili juzi, Alhamisi saa mbili usiku na alipopokea akamwambia kuwa wangesafiri wote na kuna vitu alitaka waviweke sawa lakini alishangazwa na kitendo cha mchezaji huyo kushindwa kufika katika uwanja wa ndege kwa ajili ya safari.

 

“Kwanza kabisa Morrison hatakuwepo katika mechi yetu ya kesho (leo) kwa sababu sijasafiri naye na amenikera sana kwa sababu aliniahidi jana asubuhi tungesafiri pamoja.

 

“Nilimtumia tiketi na mara ya mwisho nilimpigia simu Alhamisi, saa mbili usiku akaniambia tutaondoka wote kwa sababu kulikuwa na vitu aliniambia ingebidi tuvijadili lakini nimeshangaa asubuhi hakuja katika uwanja wa ndege, sasa kwa kuwa hajaja na mimi sitakuwa na chochote cha kujadili na yeye,” alisema Eymael.

 

MORRISON ATOA MAZITO

Baada ya kocha kuzungumza hayo, Championililimsaka Morrison ambaye ni kipenzi cha Wanajangwani ambapo alikiri kutosafiri na Eymael kwenda Shinyanga kwenye mechi kwa hofu ya kujitonesha. Mshambuliaji huyo alipata majeraha hayo kwenye mchezo wa kirafiki waliocheza na Transit Camp kwenye Uwanja wa Chuo cha Sheria, Ubungo jijini Dar es Salaam.

 

“Nimepona majeraha yangu ya goti, lakini nimeona ninahitaji muda kidogo wa kuangalia maendeleo yangu zaidi kwa siku mbili huku nikiendelea na mazoezi ya binafsi.

 

“Nilitamani kusafiri kwenda Shinyanga kucheza dhidi ya Mwadui, lakini nikahofia kujitonesha majeraha yangu, kikubwa nataka kuwepo katika sehemu ya kikosi kitakachocheza na JKT Tanzania (Jumatano ijayo).

 

“Hivyo, wakati timu inatoka Shinyanga kuja kucheza Dodoma, mimi nitaanza safari ya kuelekea huko kwenda kuungana na kikosi kwa ajili ya mchezo dhidi ya JKT,” alisema Morrison

Stori na Abdulghafal Ally, Dar es SalaamToa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *