Mtoto Mkubwa wa Sokoine Kuzikwa Kesho Monduli

MTOTO wa kwanza wa waziri mkuu wa zamani, Edward Moringe Sokoine, Lazaro Sokoine (pichani kushoto), aliyefariki dunia Jumamosi Machi 28, 2020 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, anatarajiwa kuzikwa kesho Jumanne Machi 31, Monduli Juu mkoani Arusha.

 

Msemaji wa familia ya Sokoine, Namelock Sokoine, amesema mwili wa marehemu Lazaro utasafirishwa leo Jumatatu Machi 30 kwenda Monduli na maziko yatafanyika kesho Jumanne nyumbani kwao Monduli Juu.

 

Kuhusu kifo chake, kaka wa  marehemu, Balozi Joseph Sokoine,  amesema Lazaro alianza kutibiwa maumivu ya kifua katika Hospitali ya Rufaa Morogoro kabla ya kuhamishiwa Muhimbili ambako mauti yamemkuta.

 

“Aliugua kifua kwa muda mrefu… pafu moja liliharibika na kushindwa kufanya kazi kabisa,” alisema.

 

Lazaro ni miongoni mwa watoto 11 wa marehemu Edward Sokoine, sita wa mke mkubwa, Napono;  watano wa mke mdogo, Nekiteto.

 

Lazaro aliyekuwa anaishi Morogoro kwa shughuli zake za kijasiriamali, alizaliwa Enguiki, Monduli – Arusha Machi 13, 1961 na ameacha watoto wawili.

 
Toa comment