Mugalu, Kagere Wampa Sven Kiburi Kwa Yanga

KASI ya ufungaji ya mastraika wawili wa Simba, Chris Mugalu na Meddie Kagere imempa kiburi kocha wa timu hiyo, Sven Vandenbroeck, huku akisema atashinda mechi yoyote kwa sasa.

 

Simba na Yanga wamebakiza michezo miwili miwili kabla hajawavaana Oktoba 18 kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, mechi ambayo inaonekana inaweza kumaliza ubishi kati yao.

 

Pamoja na kwamba kocha huyo hakuitaja Yanga moja kwa moja, lakini amesema kuwa atashinda kila mchezo wa ligi akimaanisha pamoja na huo wa Yanga.

Kocha huyo amesema kuwa wachezaji wake hao pamoja na wengine wanaocheza eneo la ushambuliaji akiwemo Bernard Morrison, wanampa uhakika wa kushinda kwenye mechi yoyote ile kwani nje ya kufunga wanajua kutengeneza nafasi.

 

Mugalu na Kagere wote kwa sasa wamefunga mabao mawili kwenye ligi wakiwa sawa na kiungo Mzambia, Clatous Chama na Mzamiru Yassin.Sven ameliambia Championi Jumatano,kuwa uwezo huo wa juu wa kufunga wa mastraika wake hao unampa mwanga wa kuona ana uwezo wa kushinda mechi yoyote bila ya kujalisha ni ya ligi au ya kimataifa.

 

“Tuna washambuliaji wengi wazuri ambao wanajua kwa kiasi kikubwa kufunga, kitu ambacho ni kizuri kwangu kwa sababu hatutegemei mtu mmoja kwenye hilo.

“Wanacheza kitimu na kupeana nafasi ambazo zinatufanya tuwe na uhakika wa kushinda kwenye mechi yoyote ile iwe ya ligi au kimataifa ambapo tuna miezi michache kabla ya kuanza kupambana,” alimaliza Sven.

 

Timu hiyo imecheza michezo minne ya ligi na kufanikiwa kushinda mitatu na kutoka sare mchezo mmoja ambapo kwa sasa ina pointi 10 sawa na Yanga lakini ikiwa nafasi ya pili kutokana na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Stori: Said Ally, Dar es Salaam
Toa comment