Ndoa Mpya Ya Stamina Yanukia

33 0

Ndoa Mpya Ya Stamina Yanukia

MWANAMUZIKI wa Bongo Fleva, Bonivanture Kabongo ‘Stamina’ ameeleza kuwa baada ya ndoa yake ya kwanza kuvunjika, kwa sasa yupo mbioni kuingia kwenye ndoa nyingine kwa kuwa yeye ni mwanaume aliyekamilika.

 

Stamina ambaye ana ngoma kadhaa kama Kabwela, Mwambie, Najuta kubalehe, Nitampigia na nyingine nyingi zikiwemo zile alizofanya na Kundi la Rostam akiwa na msanii Roma Mkatoliki, alisema hayo kwenye mahojiano maalum na Showbiz Xtra na kufunguka mengi yafuatayo;

 

SHOWBIZ: Tanzania na dunia kwa ujumla imekumbwa na janga la Virusi vya Corona, unalizungumziaje?

STAMINA: Hili janga ni letu sote ambalo linatesa dunia nzima na vitu vingi vimesimama, hivyo tunatakiwa kumshukuru Mungu tu.

SHOWBIZ: Unazungumziaje kwa upande wa muziki maana kazi nyingi za wasanii zimesimama kutokana na janga hili?

 

STAMINA: Kiukweli hali ni ngumu sana maana wasanii wengi tunategemea shoo ila cha muhimu ni kusubiri tu hali ikae sawa maana hili jambo ni la kupita, yote yatapita na mambo yatakaa sawa.

SHOWBIZ: Baada ya ndoa yako kuvunjika, upo katika uhusiano mpya?

 

STAMINA: Ndiyo niko katika uhusiano maana kama mwanaume rijali, nisingeweza kuishi bila mpenzi.

SHOWBIZ: Je, una mpango wa kufunga ndoa tena au ndiyo basi?

STAMINA: Maisha hayawezi kusimama, lazima yaendelee na mwanaume anayekuwa katika uhusiano lazima ategemee ndoa, hivyo watu wategemee lolote.

SHOWBIZ: Ndoa yako ilikuwa ni ya Kikatoliki na tunajua ni ndoa moja tu huruhusiwi ndoa zaidi ya moja. Je, hapa itakuwaje?

STAMINA: Maandiko siku zote hayabadiliki, nakubali hilo suala lipo katika ukatoliki lakini ndiyo tayari ndoa ilishavunjika, hali itabaki kuwa hivyo ilivyo maana siwezi kubaki katika uzinifu siku zote.

 

SHOWBIZ: Dhamira yako ni nini mpaka ukaamua kuandaa makala ya Kivuli cha Ndoa?

STAMINA: Siyo kila mtu anapenda kusikiliza muziki, wengine wanapenda kusoma na wazo la Asiwaze lilikuwa likizungumzia uhalisia katika ndoa yangu iliyopita, hivyo hata kuandaa makala hiyo ni kufanya watu wajifunze kupitia maandishi.

 

SHOWBIZ: Wewe na Roma mlikuwa mkitengeneza pacha nzuri sana, lakini sasa Roma anaishi Marekani. Vipi kundi lenu la Rostam bado lipo?

STAMINA: Niwatoe shaka mashabiki kuwa, Rostam bado ipo na tunaendelea kutoa kazi kama kawaida, japokuwa Roma anaishi Marekani, lakini tunarekodi ngoma kama kawaida maana hata huko pia kuna studio.

 

SHOWBIZ: Kwa mwaka huu masuala ya album yamekaaje kwa upande wako?

Stamina: Msanii ili uwe wa kimataifa, ni lazima utoe album, maana singo hazimtambulishi msanii bali anatambulishwa na album, hivyo mipango ipo hata kama mauzo yanasumbua.

 

SHOWBIZ: Rostam nikimaanisha wewe na Roma mnaonekana kutetereka katika ndoa zenu. Je, mnafeli wapi?

STAMINA: Naweza kuzungumzia upande wangu, kuhusiana na Roma na mkewe siwezi kusema kitu, ingekuwa umemuuliza Roma kuhusu ndoa yangu angezungumza kwa sababu wao ndiyo walisimamia ndoa yetu.

 

SHOWBIZ: Vipi kwa upande wako, sasa unaitazamaje siasa maana naona kuna baadhi ya wasanii wa Hip Hop wako kwenye siasa mfano mzuri ni Mhe Sugu, na Profesa Jay, wewe ulishawahi kuwaza kugombea kwenye kipindi hiki cha uchaguzi?

 

STAMINA: Masuala ya siasa na mimi ni vitu viwili tofauti, sijawahi kuwaza kuingia kwenye siasa ila ikatokea watu wakataka kunichagua niwaongoze, niko tayari ila siyo mimi kuwafuata kuomba kura.

SHOWBIZ: Mashairi mnayotumia kwenye ngoma zenu huwa ni magumu sana, vipi mnapitia changamoto yoyote?

 

STAMINA: Unajua moja kati ya nguzo za Hip Hop ni ukweli kwa hiyo unapofanya aina ya nyimbo kama hizi, lazima useme ukweli hata kama mtu hajapenda au kapenda, lakini ilimradi ujumbe ufike tu.

SHOWBIZ: Wasanii wengi sasa hivi wamekuwa wakibadili ladha ya muziki wao. Je, kwa upande wako ushawahi kuwaza kuimba Singeli.

 

STAMINA: Kwa upande wangu mimi nafanya muziki mmoja tu wa Hip Hop, kwenye suala la Singeli siwezi kufanya kwa sababu siyo mpenzi wa Singeli, ni mpenzi wa Hip Hop tu.

SHOWBIZ: Ni mafanikio gani unayojivunia kupitia muziki?

 

STAMINA: Kwangu mafanikio ninayojivunia ni fikra, mali si mafanikio, hayo ni mahitaji, lazima mtu awe nayo lakini mafanikio makubwa ni ya fikra, ukiweza kujenga watu wakakuamini, hata kwenye shoo inatosha.

SHOWBIZ: Neno la mwisho kwa mashabiki zako watarajie nini kutoka kwako?

STAMINA: Watarajie vitu vingi kutoka kwangu kikubwa wazidi kunisapoti.

MAKALA: KHADIJA BAKARI NA HAPPYNESS MASUNGA
Toa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *