Pacha Zitakazotisha Ligi Kuu Bara 2020/2021

3 0Pacha Zitakazotisha Ligi Kuu Bara 2020/2021

LIGI Kuu Bara inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba 6, huku msimu huu tukizishuhudia jumla ya timu 18 zikipambana kuwania ubingwa ambao unashikiliwa na Simba kwa msimu wa tatu mfululizo. Timu za Dodoma FC, Gwambina na Ihefu zikionja kwa mara ya kwanza ladha ya Ligi Kuu Bara baada ya kupanda daraja.

 

Gazeti lako bora la michezo na burudani Championi Jumatatu linakuletea baadhi ya pacha ambazo zitatikisa zaidi kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu kutokana na usajili ambao unaendelea kufanyika hadi sasa…

 

CLATOUS CHAMA, LUIS MIQUISSONE NA BERNARD MORRISON-SIMBA

Ni moja ya pacha ambazo zinasubiriwa kwa hamu kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu kutokana na uwezo mkubwa wa wachezaji hao. Hii inatarajiwa kuwa moja ya pacha tishio kwenye safu ya kiungo cha ushambuliaji ndani ya timu hiyo, Morrison anaungana na Miqussone na Chama baada ya kukamilisha dili lake la kujiunga na Simba kwa miaka miwili akitokea Yanga SC.

 

BAKARI MWAMNYETO NA LAMINE MORO-YANGA

Msimu uliopita, safu ya ulinzi ya Yanga iliruhusu jumla ya mabao 28 kwenye mechi 38, hivyo basi usajili wa Mwamnyeto kutoka Coastal Union unatarajiwa kutengeneza safu imara ya ulinzi kwa kushirikiana na beki kisiki wa timu hiyo, Lamine Moro.

 

VITALIS MAYANGA NA YUSUPH MHILU-KAGERA

Kagera Sugar imefanikiwa kumbakisha kikosini nyota wake Yusuph Mhilu huku wakimuongeza kikosini mshambuliaji wa zamani wa Ndanda, Vitalis Mayanga.

Mhilu ameifungia Kagera Sugar jumla ya mabao 13 kwenye Ligi Kuu Bara huku Mayanga akimaliza msimu na mabao saba kwenye ligi hiyo, uwezo wa nyota hawa unatarajiwa kutengeneza moja ya pacha hatari zaidi kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, ukiachana na uwezo wa kufunga, pia nyota hawa wana uwezo mkubwa wa kutengeneza pasi za mabao.

 

AWESU AWESU, ABUBAKAR SALUM NA ALLY NIYONZIMA –AZAM

Azam FC pia ni miongoni mwa timu ambazo zimefanya usajili wa uhakika msimu huu kwa kuwaongeza kikosini nyota kadhaa akiwemo Mnyarwanda Ally Niyonzima na kiungo Awesu Awesu aliyejiunga na timu hiyo akitokea Kagera Sugar.

 

Viungo hawa wanatarajiwa kutengeneza pacha bora kwenye kikosi chao ukizingatia wote ni wachezaji wenye uwezo mkubwa, Sure Boy amekuwepo ndani ya kikosi cha Azam kwa miaka takriban 12, hivyo basi kuongezeka kwa Awesu na Niyonzima kutaongeza ubunifu kwenye safu ya kiungo ya timu hiyo na kuifanya kuwa moja ya pacha hatari na za kuchungwa zaidi kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.

 

LUCAS KIKOTI, ABDULHALIM HUMUD NA SIXTUS SABILO-NAMUNGO

Sabilo alikuwa kwenye kiwango bora akikipiga kwenye kikosi cha Polisi Tanzania akitengeneza pacha matata na Marcel Kaheza, kuwepo kwake ndani ya Namungo akishirikiana na Adulhalim Humud na Lucas Kikoti inatarajiwa kuwa moja ya pacha hatari zaidi kwenye Ligi Kuu Bara msimu ujao.

 

IBRAHIM AME NA JOASH ONYANGO-SIMBA

Ingizo jipya ndani ya Simba, Ame na Onyango ni moja ya mabeki wenye uwezo mkubwa na wanatarajiwa kutoa upinzani mkali kwa wakongwe Paschal Wawa na Erasto Nyoni ndani ya Simba, Onyango amejiunga na Simba akitokea Gor Mahia ambapo alifanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu Kenya msimu wa 2018/19.

 

Ame amejiunga na Simba akitokea Coastal Union alipokipiga kwa mafanikio makubwa msimu uliopita, endapo watafanikiwa kuingia kwenye kikosi cha kwanza ndani ya Simba inatarajiwa kuwa moja ya pacha kali zaidi Ligi Kuu Bara msimu ujao.

 

JACOB MASSAWE NA PAUL NONGA-GWAMBINA

Gwambina FC imefanikiwa kuinasa saini ya nahodha wa zamani wa Lipuli FC Paul Nonga kwa kandarasi ya mwaka mmoja, Nonga amemaliza msimu akiwa na mabao 10 kwenye Ligi Kuu Bara, huku Massawe akitwaa tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza.

 

Nonga na Massawe wanatarajiwa kutengeneza pacha kali ya utupiaji mabao ndani ya kikosi hicho kwenye Ligi Kuu Bara msimu ujao kutokana na nyota hao kuwa na uwezo mkubwa wa kutupia mabao.

 

ZAWADI MAUYA, FEISAL SALUM NA HARUNA NIYONZIMA-YANGA

Safu ya kiungo ya Yanga msimu ujao inatarajiwa kutawaliwa na viungo wanyumbufu na wenye uwezo mkubwa wa kusakata kabumbu.

 

Ongezeko la Mauya ndani ya kikosi cha Yanga linatarajiwa kuongea ubunifu kutokana na uwezo wa kiungo huyo, uwepo wa Niyonzima na Fei Toto kwa kiasi kikubwa unatarajiwa kutengeneza pacha matata kwenye eneo la kiungo la timu hiyo kwa msimu ujao.

 

AYOUB LYANGA, OBREY CHIRWA NA NEVER TIGER-AZAM

Ongezeko la Lyanga kwenye safu ya ushambuliaji ya Azam FC, linatarajiwa kutengeneza pacha kali ya utupiaji mabao ndani ya kikosi hicho. Lyanga alimaliza msimu akichangia mabao 15 ya Coastal Union, akifunga mabao nane na asisiti saba.

 

Uwezo wa washam­buliaji wa Azam Obrey Chirwa aliyemaliza na mabao 12 na Never Tigere ambaye am­emaliza na mabao manne, unatarajiwa kutengeneza safu kali ya ushambuliaji ndani ya VPL msimu ujao na inatarajiwa kuwa moja ya safu za kuchungwa zaidi msimu ujao.

HUSSEIN MSOLEKA, Dar es SalaamToa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *