S2Kizzy Aanika Ugumu Kufanya Kazi na Mondi!

14 0S2Kizzy Aanika Ugumu Kufanya Kazi na Mondi!

KWENYE kundi la watayarishaji wa muziki (producers) Bongo na wenye ubunifu na kipaji cha hali ya juu, huwezi kumwacha Zombie.

 

Salmin Rashid Kassim almaarufu S2kizzy au Zombie, ni prodyuza aliyeliteka soko la muziki kwa sasa kwa kutengeneza ngoma kali kutoka kwenye studio zake za *****, zenye maskani yake pale Sinza- Mapambano jijini Dar.

 

S2kizzy amekuwepo kwenye gemu kwa muda mfupi, lakini kwa ngoma kali alizozipika, utadhani yuko muda mrefu.

 

Ametengeneza ngoma nyingi za wasanii kama Country Boy, Weusi na kubwa kuliko ni kutoka kwa wasanii wa Lebo ya Wasafi zikiwemo ngoma kali za bosi wa lebo hiyo kubwa ya muziki barani Afrika, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

 

Ngoma kali kama Tetema, Baba Lao, Jeje, Lavie na nyingine kibao zimepita mikononi mwake.

OVER THE WEEKEND imekusogeza karibu na S2kizzy katika mahojiano maalum (exclusive interview), ambapo anafunguka mengi ikiwemo ukaribu na kufanya kazi nyingi na Diamond au Mondi.

OVER ZE WEEKEND: Ni kazi ipi iliyokutambulisha kwenye gemu?

S2KIZZY: Kazi ambazo zilinitambulisha, nilifanya na Country Boy kama Hakuna Matata, Turn Up na nyingine nyingi ambazo zinafanya vizuri.

OVER ZE WEEKEND: Ni ugumu gani ambao ulipitia kipindi unaanza kazi ya uprodyuza?

S2KIZZY: Ugumu mkubwa ilikuwa ni mazingira magumu ya kufanyia kazi na kuwapata wasanii.

OVER ZE WEEKEND: Umefanya kazi nyingi na wanamuziki wakubwa, je, nini siri nyuma ya pazia?

S2KIZZY: Kikubwa ni kujituma, kufanya kazi kwa bidii na ubunifu. Ili mtu ufanikiwe, lazima utafute vitu vipya. Pia kemistri ya wasanii inafanya hata ngoma zikitoka ziwe na mapokeo makubwa.

OVER ZE WEEKEND: Unadhani kuwa prodyuza bora, lazima kuzingatia nini?

S2KIZZY: Kwanza unatakiwa umfanye msanii awe huru kufanya kazi na wewe na upya kwenye kazi zako.

OVER ZE WEEKEND: Wewe ni prodyuza, pia unaimba, je, unameneji vipi muda wako?

S2KIZZY: Mimi si msanii kabisa, hata ikitokea nimeimba, basi nimeshirikishwa maana ndoto yangu ni utayarishaji wa muziki na ninapenda sana.

OVER ZE WEEKEND: Je, una mpango wowote wa kutoa ngoma zako mwenyewe?

S2KIZZY: Sina uhakika kwa sababu muda wangu mwingi nimewekeza kwenye kutayarisha muziki.

OVER ZE WEEKEND: Umefanya kazi nyingi za wanamuziki wa Wasafi hasa Mondi, je, koneksheni ipo vipi hapo?

S2KIZZY: Ni kuonekana kwa bidii za kazi na siwezi kusema kufanya kazi na Diamond ni kwa sababu ya ukaribu, yule ni mwanamuziki mkubwa na anapenda kazi nzuri na mafanikio makubwa.

OVER ZE WEEKEND: Mondi ni mwanamuziki mkubwa, je, ni ugumu gani unaopitia kufanya naye kazi?

S2KIZZY: Naweza kusema ugumu upo kidogo kwa sababu anapenda vitu vyake viwe bora, si changamoto sana kwa sababu anapenda vitu vipya na ujitume kufanya naye kazi.

OVER ZE WEEKEND: Je, mliwahi kugombana na Diamond kwenye masuala ya kazi?

S2KIZZY: Hapana na hakuna kitu kama hicho.

OVER ZE WEEKEND: Tangu umeanza kufanya kazi na Mondi, ni kipi unaweza kujivunia?

S2KIZZY: Faida ni nyingi sana, Diamond ni mwanamuziki mkubwa, kuwa naye karibu anakufanya ung’ae na kuonekana hata nje ya Bongo, maana anafuatiliwa na watu wengi duniani.

OVER ZE WEEKEND: Vitu gani umezidi kujifunza kuwa karibu na Mondi?

S2KIZZY: Kufanya naye kazi kumenifanya kujua vitu vingi na hata koneksheni pia maana anajua vitu vingi sana na hata ujuzi unabadilika kama prodyuza.

OVER ZE WEEKEND: Je, kufanya kazi na Wasafi, ni makubaliano ya kuwa chini ya lebo hiyo au?

S2KIZZY: Wasafi ni familia yangu, hivyo nafanya kazi kama familia maana bado hatujawa kwenye mikataba na tunasaidiana kwenye vitu vingi tu.

OVER ZE WEEKEND: Mikakati iko vipi kufanya kazi na wasanii wa kimataifa?

S2KIZZY: Mikakati ni mingi maana wanamuziki wengi wananitafuta na hiyo inafanya mimi kukua zaidi.

OVER ZE WEEKEND: Ni wanamuziki gani ambao umefanya nao kazi kimataifa zaidi?

S2KIZZY: Nigeria nimefanya na Davido, Burna Boy na wasanii wengine kutoka Rwanda, Afrika Kusini, Burundi na Sudan.

OVER ZE WEEKEND: Utofauti gani umeona kwenye kufanya kazi na wanamuziki wakubwa nje ya Bongo ukilinganisha na hapa kwetu?

S2KIZZY: Utofauti ni mkubwa kwa sababu kila msanii ana kazi zake na anajua jinsi anavyofanya kazi na kupitia na anakuwa na njia zake za biashara ambapo hata prodyuza, unajifunza njia nyingi kupitia huyo msanii. Pia kujifunza tamaduni mbalimbali.

OVER ZE WEEKEND: Uliwahi kushiriki baadhi ya tuzo ikiwemo Sound City za Afrika Kusini na AFRIMA za Marekani, je, uliwahi kupata ushindi kupitia tuzo hizo?

S2KIZZY: Sikupata ushindi, ila mimi ni kati ya maprodyuza ambao wanaangaliwa sana na nimechaguliwa mara nyingi kwa Afrika Mashariki.

OVER ZE WEEKEND: Je, imekupa chachu gani kwenye ufanisi wa kazi zako?

S2KIZZY: Inanifanya niendelee kujituma na kutafuta maana bado sijafika ninakotaka.

OVER ZE WEEKEND: Umefanya kazi nyingi na wakongwe wa muziki, utofauti uko wapi ukilinganisha na wasanii wa sasa?

S2KIZZY: Utofauti ni kwa kila msanii jinsi ya kufanya kazi hasa kwenye sound.

OVER ZE WEEKEND: Ishu ya maprodyuza kuiba biti za wanamuziki wa nje, kwako unaizungumziaje?

S2KIZZY: Hicho kitu kipo kwa baadhi ya watu, ila kwa upande wangu sijawahi kuiba, ukiona nimepiga biti imeendana, ni kwa sababu ndani yake kuna kitu.

OVER ZE WEEKEND: Wewe na Mondi mlipitia tuhuma ya kukopi Ngoma ya Neira Marley ya Baba Lao, hili unalizungumziaje?

S2KIZZY: Tuliongea naye na kufanya vile ilikuwa si kwa kukurupuka, japo ratiba ilibadilika akafanya Mondi tu.

OVER ZE WEEKEND: Kila kazi haikosi changamoto, je, kwa upande wako iko vipi?

S2KIZZY: Changamoto zipo hasa kwenye haki miliki, ila zingine ni za kawaida tu, tunahangaikia kupata chama cha maprodyuza.

OVER ZE WEEKEND: Muziki umekupa vitu gani vya kujivunia?

S2KIZZY: Nafuatiliwa na watu wengi kutokana na kuwa na koneksheni kubwa. Pia nahamasisha vijana.

OVER ZE WEEKEND: Ni utajiri kiasi gani ambao umeupata kupitia kazi yako?

S2KIZZY: Vitu vipo ila siwezi kuvitaja, kikubwa namshukuru Mungu kwa ninachokipata.

 MAKALA: HAPPYNESS MASUNGAToa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *