Sarpong Ataka Rekodi ya Mabao Yanga

MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga, Mghana, Michael Sarpong, amefunguka kuwa deni kubwa kwa sasa lililo mbele yake ni kuhakikisha anafunga mabao ya kutosha ili kuvunja rekodi zake za alipotoka.

 

Sarpong amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Rwanda katika Klabu ya Rayon Sport ambayo alikuwa ameshamaliza mkataba wake huku akiwa na rekodi ya kufunga mabao 23 pamoja na pasi za mwisho 13 msimu wa 2018-19, wakati msimu uliopita alifanikiwa kufunga mabao saba na pasi za mwisho tano kabla ya kuingia kwa Corona iliyokatisha ligi ya Rwanda.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, mshambuliaji huyo alisema kuwa yupo tayari kuipigania timu hiyo katika michuano hiyo kwa kuhakikisha anafunga mabao ya kutosha ambayo yataacha rekodi nyingine kubwa zaidi alizoacha nchini Rwanda.

 

“Kwanza mashabiki wanatakiwa wajue kwamba nipo tayari kwa kila kitu katika kuhakikisha Yanga inafikia malengo yake, nataka kufanya vizuri zaidi ya hata nilivyokuwa Rayon ya Rwanda, nina imani nitaweza katika hilo, sina shaka.

 

“Unajua kama sijafanya mimi, unategemea nani anaweza kufanya? Ndiyo maana nataka kuweka rekodi yangu nyingine hapa kwa kufunga mabao ya kutosha kwa lengo moja la kuona timu inafikia malengo ndani ya msimu huu, hilo ndilo kubwa ambalo naweza kuwaambia mashabiki kwa sasa,” alisema Sarpong.

IBRAHIM MUSSA, Dar es Salaam

 Toa comment