Sarpong: Nitafunga Mabao Mengi Yanga

BAADA ya kuanza vizuri katika ajira yake mpya, mshambuliaji wa Yanga, Mghana, Michael Sarpong, amefunguka kuwa ndoto yake kubwa kwa sasa ndani ya timu hiyo ni kuendelea kufunga kwa kuwa ndiyo jukumu lake kubwa.

 

Sarpong amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Rayon Sport, tayari ameanza kuwasha moto ndani ya kikosi cha timu hiyo kufuatia kufunga bao moja katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Aigle Noir ya Burundi waliocheza nao wikiendi iliyopita kwenye kilele cha Siku ya Mwananchi jijini Dar es Salaam.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Sarpong alisema kuwa bao hilo kwake limemfungulia njia ya kuendelea kufunga zaidi katika ligi kuu inayotarajia kuanza keshokutwa Jumapili kwa Yanga kucheza na Prisons.

“Binafsi nashukuru Mungu kwa sababu ilikuwa ndoto yangu kuona nafunga kwenye mchezo ule kwa kuwa ulikuwa muhimu kwa mashabiki ambao walikuja uwanjani kutusapoti, maana walikuwa wamejaa kwa sababu yetu.

 

“Lakini naamini litaniongezea chachu kubwa ya kuendelea kufanya vizuri katika ligi, kwa sababu nipo hapa kwa kazi ya kufunga mabao, maana ndiyo jukumu langu, sasa sitaki kuona nakwama kwenye hilo, kwani nataka kufunga mabao mengi zaidi, japo ni suala gumu kwa sasa kuweka mipango yangu wazi zaidi ya kuwa msaada kwenye timu,” alisema.

STORI: SAID ALLY,Dar es SalaamToa comment