Serikali yamliza Aunt Ezekiel

MASKINI! Ikiwa ni miezi miwili tu imepita tangu alipofungua pub yake kubwa ya kisasa maeneo ya Mikocheni jijini Dar es Salaam inayojulikana kwa jina la The Luxe, serikali imemliza staa wa filamu za Kibongo, Aunt Ezekiel baada ya kutakiwa kuifunga.

Akielezea chanzo cha kufungwa kwa pub hiyo, mmoja wa wakazi wa eneo hilo ambaye aliomba hifadhi ya jina lake alisema, Aunt alikuwa akifungulia muziki mkubwa kwenye pub yake na kuwa kero kwa wakazi wanaozunguka eneo hilo hivyo wakaamua kumchukulia hatua za kumshtaki msanii huyo.

Kutokana na kushtakiwa huko, Alhamisi iliyopita pub hiyo ya kisasa ilifungwa rasmi hivyo kuanzia wakati huo Aunt akawa hana ujanja tena labda akafanyie biashara hiyo sehemu nyingine.

“Kiukweli ilikuwa ni kero kubwa hapa mtaani kwetu kwani hii pub ya Aunt walikuwa wakifungulia muziki kwa sauti ya juu, iwe mchana au usiku na walikuwa hawajali kwamba wako katika makazi ya watu huenda kuna wagonjwa wa moyo ama laa, tunashukuru kwa sababu imefungwa,” alisema mtoa habari huyo.

Baada ya kupata habari hiyo, RISASI JUMAMOSI lilimtafuta Aunt ambaye alikiri kuwa ni kweli pub yake ameifunga baada ya kushtakiwa na majirani na serikali kumtaka aifunge.

Aliongeza kuwa jambo hilo limemuumiza sana kwani hata hajarudisha hata robo ya fedha alizotumia kufungulia.

“Inaniuma sana kwani nilikuwa sijapata faida hata kidogo… yaani hata fedha niliyofungulia nilikuwa sijaipata hata robo maana nilitumia fedha nyingi sana kuigharamia hiyo pub lakini ndiyo hivyo sina la kufanya nimetii amri ya serikali, nimefunga,” alisema Aunt.

STORI: IMELDA MTEMA
Toa comment