SIMBA SC YAANZA LIGI NA POINTI 21

11 0


NA WINFRIDA MTOI

SIMBA imepiga hesabu kali ya kukusanya pointi 21 katika mechi saba za mwanzo za Ligi Kuu Tanzania Bara ili kuweka mikakati ya kutetea ubingwa wao walioutwaa kwa mara tatu mfululizo.

Wekundu hao wa Msimbazi bado wanaendelea kuonesha makali waliyotoka nayo msimu uliopita baada ya kutwaa taji la Ngao ya Jamii Jumapili iliyopita.

Simba imechukua taji hilo la ufunguzi wa Ligi Kuu Bara kwa kuichapa Namungo FC mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Katika kuonesha kuwa wapo fiti, siku moja baada ya mechi hiyo, Simba ilichezesha kikosi kingine tofauti katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Arusha FC na kuishindilia mabao 6-0.

Maandalizi yote hayo ni mikakati ya kuendelea kutawala na kulinda heshima yao itakayowafanya watambe Afrika katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika watakayoshiriki mwakani.

Simba inatarajia kuanza mechi yake ya kwanza ya ligi ugenini dhidi ya Ihefu ya jijini Mbeya, huku ikitamba kushinda mechi saba mfululizo za mwanzo ili kukusanya pointi 21.

Ratiba ya Simba inaonesha kuwa baada ya kutoka Mbeya, itacheza na Mtibwa Sugar kisha inarejea Dar es Salaam kucheza na Biashara United na Gwambina FC.

Mechi nyingine itakutana na Tanzania Prisons ugenini, kisha kuingia katika mtanange wa ‘derby’ dhidi ya watani wao Yanga.

Kocha mkuu wa timu hiyo, Sven Vandenbroeck, aliweka bayana kuwa wana kazi kubwa kuhakikisha wanafikia malengo ya klabu hiyo ikiwamo kutetea taji lao.

Alisema hali hiyo inatokana na timu nyingi kufanya maandalizi mazuri ya kusajili wachezaji wenye viwango tofauti na msimu uliopita.

Kikosi hicho tayari kimewasili jijini Mbeya kwa maandalizi ya mchezo wake na Ihefu, utakaochezwa Jumapili, Uwanja wa Sokoine Mbeya.Source link

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *