Simba Waambiwa Dau la Mwamnyeto Ni Milioni 100

HABARI ndiyo hiyo. Uongozi wa Coastal Union umeweka wazi dau la milioni 100 ambalo kama litafikiwa na timu yoyote basi watamuachia beki wao wa kati, Bakari Nondo Mwamnyeto.

 

Mwamnyeto ambaye ni nahodha wa timu hiyo, amekuwa akihusishwa kusajiliwa na klabu za Simba, Yanga na Azam kwa ajili ya kutaka kuviboresha vikosi vyao katika sehemu ya eneo la ulinzi.

 

Chanzo chetu cha kuaminika ndani ya Coastal Union kimeliambia Championi Jumatatu kuwa, timu hiyo ipo tayari kumuachia beki huyo kama kuna timu yoyote ambayo itafikia dau la milioni 100 kwani hapo awali ilizikataa milioni 85 za moja ya timu ambayo ilipeleka awali.

 

“Hapo awali uongozi wa Coastal ulipelekewa ofa ya milioni 85 na moja kati ya timu ambazo zilikuwa tayari kwa ajili ya kumsajili beki huyo lakini waliigomea pesa hiyo wakitaka iongezwe ili kufikia angalau milioni 100 ambayo wangekuwa tayari kumuachia.”

 

Kwa upande wa beki huyo, alipotafutwa kuzungumzia thamani ya dau lake, alisema kuwa hajaruhusiwa kuzungumza kitu chochote kuhusiana na usajili wake kwani kila kitu kipo chini ya viongozi wake.

 

“Kila kitu kuhusu masuala ya usajili nimeuachia uongozi wangu hivyo haitakuwa sawa mimi kuzungumza chochote kuhusu usajili wangu labda kama ikitokea mambo ya usajili yamekamilika,” alisema Mwamnyeto.

 

MARCO MZUMBE | Dar es Salaam
Toa comment