Tundu Lissu Amlilia ‘Mr White’ ”Alikuwa Mtu Mwema”

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu  leo Septemba 15, 2020 ametoa pole na kutuma salamu za rambi rambi kufuatia kifo cha Salim Abdullah Turky ‘Mr White’ ambaye alikuwa mbunge aliyemaliza muda wake katika jimbo la Mpendae, Unguja kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

”Usiku wa leo nimepokea taarifa za msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Mpendae, Salim Turky, “Siku ambayo nilishambuliwa kwa risasi Dodoma Septemba 7 2017, Mheshimiwa Turky alitoa dhamana ya fedha kuhakikisha nasafirishwa kwa ndege kwenda Nairobi kwa matibabu ya dharura na kuwa mtu muhimu kwenye kuokoa maisha yangu.

 

“Ile ndege iliyonipeleka Nairobi – Kenya ilidhaminiwa na Salim Turky, alikuwa mtu mwema, alikuwa mtu safi, wengi wanasema kuwa kupona kwangu ilikuwa ni miujiza ya Mungu, wanasema kwa usahihi kabisa. Salim Turky alichangia muujiza huo, leo napenda kutoa salaam za pole kwa ndugu jamaa na familia yake, Mwenyezi Mungu awatie faraja na nguvu kwa msiba huu,” ameyasema Lissu katika mkutano wake wa kampeni kwenye Uwanja wa Barafu, Rujewa, wilayani Mbarali.



Toa comment