UJENZI UWANJA YANGA WAANZA KIMYAKIMYA

22 0


NA TIMA SIKILO

KAMA masihara, Yanga nao mdogomdogo wameanza hatua za awali za ujenzi wa uwanja wao uliopo eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Uwanja huo waliupata kama zali baada ya kupewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, wakati walipofanya mkutano maalumu kwa ajili ya kuichangia klabu hiyo uliojulikana kama ‘Kubwa Kuliko’.

Jana zilisambaa picha katika mitandao ya kijamii zikionyesha tingatinga liking’oa miti na kusawazisha eneo hilo ambapo baadaye Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Fredrick Mwakalebela, akakiri kwamba huo ndiyo unaotarajiwa kuwa uwanja wao mpya.

Mwakalebela alisema zoezi hilo limeanza kimya kimya ikiwa ndiyo utaratibu wao wa kutotangaza kila jambo na badala yake kusubiri watu waone.

“Ndiyo, hizo picha ni za uwanja wetu wa Kigamboni na sio Jangwani, umeshaanza kufanyiwa ukarabati wa awali,” alisema.

Kwa upande wa mkandarasi anayeshughulikia ujenzi huo, Injinia Bahati Mwasenga, alisema ni kweli wameanza kuufanyia tathmini uwanja huo ikiwa ndiyo hatua za awali za ujenzi wa viwanja vya soka duniani.

Hata hivyo, Injinia Mwasenga alisema hajajua itachukua muda gani ujenzi huo kukamilika kwasababu ndiyo kwanza wameanza kuchukua vipimo ambavyo vitawapa uhakika wakutoa tathmini kuhusu idadi ya watu ambao wanaweza kuingia kwenye uwanja huo.

“Ni kweli mimi naushughulikia uwanja huo wa Kigamboni lakini bado ni mapema kuzungumzia juu ya ujenzi kwasababu ndio kwanza mipango inaanza,” alisema Injinia Mwasenga.Source link

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *