Vita ya Chadema, NCCR Mageuzi Kilimanjaro Furaha kwa Kunguru

7 0Vita ya Chadema, NCCR Mageuzi Kilimanjaro Furaha kwa Kunguru

TANGU kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi, mkoa wa Kilimanjaro umekuwa ngome ya upinzani kwa kupitia vyama vya NCCR Mageuzi na Chadema, ambavyo vimetoa wakati mgumu kwa CCM kujinafasi katika majimbo tisa ya mkoa huo.

 

Awali NCCR Mageuzi ilishika hatamu katika mkoa huo kutokana na umaarufu wa aliyekuwa mgombea urais mwaka 1995, Agustine Mrema (Vunjo).

 

Ilhali baadaye Chadema nayo ilijimwambafai baada ya kuuweka kando ufalme wa NCCR Mageuzi kwa kupitia Freeman Mbowe (Hai) ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho.

 

Mwaka 1995, NCCR-Mageuzi ilibeba majimbo matano ya Hai, Siha, Moshi Vijijini, Vunjo na Moshi Mjini; CCM ilichukua majimbo ya Mwanga, Same Mashariki na Same Magharibi, ilhali Chadema ikiambulia Rombo.

 

Mwaka 2000, CCM ilifanikiwa kukomboa majimbo ya Rombo na Vunjo, na mwaka 2005 CCM ilifanya kazi ya ziada baada ya kufanikiwa kubeba majimbo yote isipokuwa Moshi Mjini ambalo lilikuwa ngome ya Philemon Ndesamburo (Chadema).

 

Mwaka 2010, Chadema ilifanikiwa kurejesha majimbo mawili ya Rombo na Hai na kutetea jimbo la Moshi Mjini, lakini 2015, upinzani uliweka rekodi ya kipekee baada ya kunyakua majimbo saba kati ya tisa.

 

Aidha, mwaka 2020 ndiyo mwaka ambao upinzani unakwenda kwenye uchaguzi mkuu huku kukiwa na mgawanyiko unaoweza kutoa nafasi kwa CCM kurejesha baadhi ya majimbo.

Mgawanyiko huo umetokana na ngome za upinzani kutofautiana kiasi cha wagombea wa Chadema ambao walikuwa wabunge kuhamia NCCR Mageuzi.

 

VUNJO

Katika jimbo hilo, upinzani mkali unatarajiwa kuwa kati ya vyama vinne; CCM, NCCR Mageuzi, Chadema na TLP. Hata hivyo, macho na masikio ya wengi, yameelekezwa zaidi kwa wagombea wa CCM na NCCR Mageuzi kutokana na historia ya jimbo hilo.

Tayari CCM imempitisha Dk. Charles Kimei ambaye alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB. Dk. Kimei utendaji wake umemuweka karibu na Rais John Magufuli kiasi cha kumuahidi kumpa kazi serikali kutokana na mafanikio ya ukuaji wa benki hiyo.

 

Hata hivyo, ndoto ya Dk. Kimei kupata kazi serikalini baada ya kustaafu CRDB, inaweza kuyeyuka kwa kuwa mgombea wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, naye amejipanga vilivyo kutetea jimbo hilo.

Aidha, Mgombea wa Chadema; Grace Kiwelu, naye si wa kubeza kutokana na uzoefu wake katika siasa baada ya kuhudumu katika nafasi ya ubunge wa viti maalumu kuanzia mwaka 2010 hadi sasa.

 

Vilevile, Mzee wa Kiraracha- Agustine Mrema ambaye ni mmoja wa makada waliowahi kutikisa katika jimbo hilo, naye anawania kupitia TLP.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Mrema aliangushwa na Mbatia baada ya kulitumikia kuanzia mwaka 2010 hadi 2015.

 

Kutokana na mazingira hayo, upo uwezekano mkubwa wa Dk. Kimei (CCM), kushinda kirahisi kutokana na vita ya kihistoria kati ya mafahari wawili yaani Mrema na Mbatia.

SIHA

Katika jimbo la Siha, ushindani ni kati ya vyama viwili pekee, yaani CCM na Chadema. Ikumbukwe kuwa Dk. Godwin Mollel ambaye ndiye mgombea wa CCM aliyepitishwa baada ya kumuangusha Agrey Mwanri katika kura za maoni, bado anaweza kupata ushindani mkubwa hasa ikizingatiwa Mwanri ni mmoja wa makada wanaokubalika katika jimbo hilo, kwani katika kura za maoni walipishana kura moja tu (148,147) na Mollel.

 

Licha ya kwamba Dk. Mollel atapambana na Elvis Mos (Chadema), bado Dk. Mollel atapambana na vivuli viwili, kwamba atapambana na Chadema pamoja na makada wa CCM ambao wanamuunga mkono Mwanri.

 

Makada hao wa CCM wanaweza kumpigia Mos kura za hasira hasa ikizingatiwa kuwa, awali Dk. Mollel alikuwa CCM baada ya kutoswa katika kura za maoni mwaka 2015, akakimbilia Chadema ambako upepo wa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa ulimbeba na kupata ubunge, lakini baadaye alirejea CCM pamoja na ubunge wake.

 

Hii inaleta picha kwamba, bado wapo wanaCCM akiwamo Mwanri ambaye alipambana naye mwaka 2015, ambao wanamtazama Dk. Mollel kwa jicho tofauti, ndiyo maana alimpa upinzani mkali katika kura za maoni.

 

Hata hivyo, sanduku la kura ndilo litakaloamua matokeo ya uchaguzi huo kwani Dk. Mollel ni moja ya makada watatu wa upinzani waliohamia CCM na kupitishwa kuwa wagombea ubunge.

MOSHI VIJIJINI

Hili ni moja ya jimbo ambalo lina mfanano na Vunjo au Rombo, kwa sababu wagombea watatu wa jimbo hilo Prof. Patrick Ndakidemi (CCM), Lucy Ndesamburo (Chadema) na Anthony Komu (NCCR Mageuzi) wote wana nafasi sawa za kushinda.

 

Prof Ndakidemi licha ya kuwa mchanga katika siasa za jimbo hilo, anaweza kubebwa na mpambano unaoenda kunoga kati ya Lucy na Komu kwa sababu watagawana kura.

 

Kwamba Komu ambaye alikuwa Chadema na kuhamia NCCR Mageuzi, bado ataweza kuwa na wafuasi wake ilhali Lucy naye ambaye inadaiwa kuwa misingi imara katika jimbo hilo naye, pia anaweza kujimwambafai.

 

Jitihada za Lucy kuwania jimbo hilo, hazikuanza leo, ndiyo maana zipo taarifa kuwa alimshinda Komu katika kura za maoni ndani ya Chadema mwaka 2015.

 

Hata hivyo, nguvu ya fedha na kukubali kwa Lucy, kunaweza kumwangusha Komu na kusababisha mpambano kuwa mkali kati ya Chadema na CCM.

 

HAI

Salasisha Mafue ndiye mgombea wa CCM, licha ya kwamba kumekuwapo na rafu nyingi tangu Mkuu wa Wilaya hiyo, Lengai Ole Sabaya atue, bado Freeman Mbowe anatajwa kuwa na nguvu ya kipekee kutokana na misingi imara aliyojiwekea kuanzia kwenye ngazi ya viongozi wa dini, wazee na akina mama.

 

Hata hivyo, Mafue hana jina maarufu kama ilivyo kwa Mbowe, badala yake anatarajiwa kubebwa na Sabaya ambaye amejipambanua kutumia mbinu nyingi za kisiasa kumdhoofisha Mbowe.

 

Pamoja na hayo, Mbowe hawezi kukubali kirahisi kuachia jimbo hilo na kubeba aibu ya kuwa kiongozi wa chama aliyeangushwa jimboni kwake hasa ikizingatiwa amelikumbatia tangu mwaka 2010.

ROMBO

Jimbo hilo nalo limekumbwa na jinamizi la Chadema na NCCR Mageuzi kuvurugana. Kwa maana hiyo, Prof. Adolf Mkenda (CCM) atakumbana na upinzani mkali kutoka kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Joseph Selasini (NCCR Mageuzi) na Patrick Assenga (Chadema).

 

Licha ya kwamba Prof Mkenda hana historia kubwa katika uwanda wa siasa zaidi ya kuwa Katibu Mkuu wizara ya maliasili na utalii, anaweza kubebwa na vita ya Selasini na Assenga.

Selasini alikuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema, tayari amejijengea jina na misingi imara ya kisiasa, lakini baada ya kuhamia NCCR Mageuzi, upo uwezekano mkubwa Chadema kumbomoa, hivyo kusababisha wawili hao kugawana kura jambo ambalo litaweza kumbeba kwa urahisi Prof. Mkenda.

MOSHI MJINI

Hii ndiyo ngome ya Chadema kwa miaka nenda rudi, hali hiyo inatokana na misingi imara iliyojengwa na Philemon Ndesamburo tajiri ambaye hakusita kutumia fedha zake kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hilo.

 

Ufalme wake katika jimbo hilo, ulidhihirika mwaka 2015 baada ya kustaafu kugombea na baadaye kumuachia Japhary Michael ambaye alishinda kirahisi kwa nguvu ya Ndesamburo.

 

Hata hivyo, sasa Ndesamburo hayupo ameshafariki, tayari aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Japhary Michael ametangaza kutogombea tena baada ya kuwepo fununu ya kutaka kufukuzwa ndani ya chama.

 

Kwa maana hiyo, Raymond Mboya (Chadema) ambaye alikuwa Meya Manispaa ya Moshi. Mboya atapambana na Priscus Tarimo (CCM) ambaye awali alikuwa Katibu wa uenezi Moshi Mjini.

 

Wawili hao ni sawa na kusema kuwa wanaanza upya, kwamba mazingira ya kisiasa yanatoa nafasi sawa kwa wote hasa ikizingatiwa Tarimo ameteuliwa baada ya kumweka kando tajiri wa mabasi ya Ibra Line, Ibrahim Shayo aliyekuwa mshindi wa pili katika kura za maono.

 

SAME MASHARIKI

Katika hali sasa Anne Kilango Malecela (CCM) anaonekana kujipanga zaidi kukomboa jimbo hilo kutoka kwa Nagenjwa Kaboyoka (Chadema) ambaye anagombea kwa mara ya pili.

 

Ikumbukwe akina mama hao wote kwa pamoja wameshaonja utamu wa jimbo hilo, kwani Kilango alikuwa mbunge kuanzia mwaka 2005 hadi 2015, baadaye akakwapuliwa na Kaboyoka mwaka 2015 hadi 2020. Hawa mpambano utakuwa mkali lakini Kilango akibebwa na kasi ya Rais John Magufuli.

SAME MAGHARIBI

Licha ya Dk. Mathayo David Mathayo (CCM) kuwa mgombea aliyeshinda kwa kura nyingi katika mkoa wa Kilimanjaro kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, sasa inadaiwa ndiye mgombea mwenye wakati mgumu kurudi jimboni kwake.

 

Ameteuliwa na CCM kupeperusha tena bendera ya chama. Amelikumbatia jimbo hilo tangu mwaka 2005 hadi sasa. Mwaka huu atapambana na Gervas Mgonja (Chadema) ambaye amejifunza siasa za mikiki baada ya kuwa Katibu wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

 

Baada ya jina la Dk. Mathayo kutangazwa maono ya wananchi wengi wa jimbo hilo yalioelezea kuhuzunishwa kwa kuwa kada huyo, wanadai ameshindwa kuendana na kasi ya Magufuli, kwamba upepo wa kisiasa umemtupa kando.

Hivyo upo uwezekano mkubwa kwa Mgonja kupata kura za hasira iwapo uchaguzi utafanyika kwa haki.

 

MWANGA

Anania Tadayo ndiye mgombea mpya wa CCM baada ya kumng’oa mkongwe Profesa Jummane Maghembe. Alimwangusha kwenye kura za maoni na sasa ameteuliwa kupambana na Henry Kilewo (Chadema) ambaye anawania kwa mara ya pili jimbo hilo.

 

Kileo anaonekana ni kijana asiyetaka kushindwa, hivyo upo uwezekano kuwa anafurahia ujio wa Tadayo kutokana na ugeni wake kwenye mikiki ya jimbo hilo. 0715126577.

NA GABRIEL MUSHIToa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *