Wabunge 21 CCM Kazi Kwao

1 0Wabunge 21 CCM Kazi Kwao

PAMOJA na Chama Cha Mapinduzi ‘CCM’ kuweka wagombea ubunge kwenye majimbo yote 264 nchi nzima, uchunguzi unaonesha kuwa wagombea 21 presha ya kushinda iko juu.

 

Wabunge hawa ni wale ambao hawakushinda kwenye kura za maoni ndani ya chama hicho tawala na majina yao kupitishwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ‘CC’. Uamuzi huo mgumu wa CC kuwapa nafasi walioshindwa ni kama kuwaambia “kazi kwao” kuupigania ushindi wa chama hicho kwa nafasi ya ubunge.

 

“Ukiangalia katika hao 21 wapo ambao hawakufika hata tatu bora kwenye kura za maoni, lakini wamepitishwa na CC.

 

“Hata ningekuwa mimi, heshima hiyo niliyopewa na chama kupeperusha bendera ya CCM kwenye nafasi ya ubunge ingekuwa nzito.

 

“Nzito kwa sababu kushindwa kwake kutakuwa na maumivu kwake na kwa chama kilichomuamini,” alisema Dk. George Kahangwa ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

 

WABUNGE AMBAO KAZI KWAO NI HAWA

Ifuatayo ni orodha ya wabunge ambao wanabeba msalaba mzito wa kukiwakilisha chama kwa heshima waliopewa na CC. Miongoni mwao ni Mchungaji Josephat Gwajima (Kawe, Dar) ambaye kwenye kura za maoni alishika nafasi ya tatu nyuma ya Furaha Jacob aliyeongoza akifuatiwa na Angela Kizigha.

 

Katika Jimbo la Temeke, Dar, Doris Kilave aliaminiwa na CC, Abbas Mtevu aliyeshika nafasi ya kwanza akiwekwa kando ambapo Hamis ‘MwanaFA (MuhezaTanga) naye alipitishwa na CC huku mshindi Balozi Adadi Rajabu akihifadhiwa kwenye hazina ya chama.

 

Mwingine ni David Silinde (Tunduma-Songwe) alishika nafasi ya pili nyuma ya mshindi Aden Mwakyonde lakini akajikuta kapewa heshima na CC kupeperusha jina. Katika Jimbo la Babati Mjini, mkoani Manyara Pauline Gekul aliyeshika nafasi ya tatu kura za maoni, alichaguliwa kuwakilisha chama kwenye jimbo hilo.

 

Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, Charles Kimei alipitishwa na Enock Koola aliyeongoza kura za maoni aliachwa. Jimbo la Shinyanga mjini Patrobas Katambi ambaye hakuingia kabisa tatu bora kura za maoni CCM naye aliula huku Cecil Mwambe, Jimbo la Ndanda mkoani Mtwara akionekana keki mbele ya mshindi Oscar Anthon Ng’ itu na Faraja Nandala aliyeshika nafasi ya pili.

 

Jimbo la Busanda mkoani Geita, Tumaini Braison Magesa ambaye hakuwemo kwenye tatu bora kura za maoni alipitishwa na Kulwa Biteko aliyeshindwa kuingizwa kwenye hazina ya matumizi ya chama kama mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais John Pombe Magufuli anavyosema.

 

Stevine Lujahuka Byabato yeye alipewa heshima na CC kwenye Jimbo la Bukoba Mjini ingawa hakushinda nafasi tatu za juu ambazo kinara wa kura za maoni alikuwa Almasoud Kalumuna.

 

Mtoto wa waziri mkuu wa zamani, Mizengo Pinda, Jofrey Mizengo Pinda yeye alipitishwa kugombea Jimbo la Kavuu mkoani Katavi licha ya mshindi kwenye jimbo hilo kuwa ni Pudensiana Kikwembe. Kwenye Jimbo la Uvinza mkoani Kigoma, Nashon Bidyanguze aliaminiwa licha ya Hasna Mwilima kuongoza kwenye kura za maoni ndani ya CCM.

 

Katika Jimbo la Kigoma Kaskazini, Assa Nelson Makanika alipitishwa na CC ingawa hakushinda kura za maoni, wakati Jimbo la Nkasi mkoani Rukwa Vincent Mbogo naye akipewa heshima na CC.

 

Kwenye Jimbo la Mbinga Mjini, Sextus Mapunda alishinda lakini Nec ikampa Jonas Mbunda aliyeshika nafasi ya pili kwenye kura za maoni. Jimbo la Namtumbo mkoani Songea, Kawawa Vita Rashid aliyekuwa mshindi wa pili nyuma ya Ngonyani Edwin alipewa nafasi hiyo adimu ambayo kwa sasa anapigania ushindi wa jumla kwenye uchaguzi mkuu ujao.

 

Katika Jimbo la Wanging’ombe mkoani Njombe, Dk. Festo John Dugange aliaminiwa zaidi kwenye ubunge kuliko Enock Kiswaga aliyewekwa kwenye hazina ya chama.

 

Mkoani Tabora, Jimbo la Kaliua, Profesa Juma Kapuya alishinda lakini Kamati Kuu ikamuondoa na nafasi yake kuchukuliwa na Aloyce Kwezi aliyekuwa mshindi wa pili. Suleiman Nchambi aliyeongoza kwa kishindo Jimbo la Kishapu mkoni Shinyanga aliambiwa asubiri nafasi nyingine za utumishi ambapo Boniface Butondo aliyeshika nafasi ya tatu akiambiwa “kazi ni kwako” kukitetea chama kwenye nafasi ya ubunge.

 

Katika Jimbo la Liwale mkoni Lindi, Zuberi Kuchauka aliyekuwa nafasi ya pili nyuma ya Faith Mitambo akipewa nafasi ya kuwakilisha chama kwenye ubunge. Naye ‘Nyoka wa Makengeza” Adrew Chenge mbunge wa zamani wa Bariadi Mashariki safari hii akiambiwa apumzike licha ya kushinda kura za maoni na nafasi yake kupewa Mhandisi Andrea Kundo.

 

USHINDI KWA JASHO NA DAMU

Kutokana na heshima hiyo, uchunguzi unaonesha kuwa, wagombea hao 21 watafanya kampeni za jasho na damu ili kuhakikisha kuwa wanathibitisha ubora wao na usahihi wa uamuzi wa CC na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

 

Kama alivyosema Dk. Kahangwa kushindwa kwao kutakuwa na maumivu pacha na pengine kuwa somo kwa Kamati Kuu iliyopitisha. Hata hivyo, wengi kati ya hao 21 walipitishwa na CC mapema kwenye kampeni zao wametamba kupata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi wa Oktoba 28 mwaka huu.

 

“Mimi hapa nashinda mapema asubuhi, sioni mtu wa kushindananaye,” alisema Mchungaji Josephat Gwajima ambaye anashindana na Halima Mdee mbunge aliyemaliza muda wake kutoka Chama cha Demkrasia na Maendeleo (Chadema).

Naye Katambi amesema hakuna uchaguzi mwepesi kwake kama huu na kwamba ushindi wa CCM mwaka huu ni kama kumsukuma mlevi.

 

USHAURI WA BURE

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema ushindi wa wagombea hao utategemea namna ambayo wataweza kuyazika makundi waliyotengeneza wakati wa kura za maoni.

 

“Kuengua washindi wakati mwingine ni kuzuri na wakati mwingine ni kubaya, msipokubaliana mtaweza kujikuta mnampa ushindi mpinzani kutokana na kusalitiana.”

 

Alisemsa Jonathan Macha mkazi wa Kawe jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, viongozi wa CCM akiwemo mwenyekiti wao Rais John Pombe Magufuli wametoa wito kwa wagombea wote walioshiriki mchakato wa kura za maoni kuvunja makundi na kuwa kitu kitu kimoja li kutetea ushindi wa chama.

 

Magufuli amesema chama kikipata ushindi na yeye akachaguliwa kuwa rais atapata nafasi nyingi za kuwapa wanachama wake walioenguliwa kwenye kura za maoni ambao amewabatiza jina la “hazina.”

MWANDISHI WETU, UWAZI

 Toa comment

Posted from

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *