WABUNGE WAIPANDISHA MZUKA YANGA DODOMA

25 0


NA JESSCA NANGAWE

KITENDO cha timu ya Yanga kukaribishwa Bungeni jijini Dodoma juzi, imekifanya kikosi hicho kupandisha mzuka na kuahidi kupata pointi tatu mbele ya timu yoyote itakayokutana nayo katika michuano ya Ligi Kuu Bara inayoendelea.

Yanga ilialikwa katika ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku timu hiyo ikipokelewa kwa shangwe na kupewa ari ya kujituma zaidi kwa vile inaweza hata kutwaa ubingwa.

Akizungumza na DIMBA Jumatano, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli, alisema morali waliopewa bungeni umezidi kuwapa hamu wachezaji kupambana uwanjani ili kupata matokeo mazuri zaidi katika michezo iliyosalia.

Ikiwa imejikusanyia alama tatu katika mchezo wao wa kwanza baada ya janga la corona pale ilipowafunga Mwadui FC bao 1-0, leo imeapa kuendeleza dozi mbele ya maafande wa JKT Tanzania.

Yanga iliyopo chini ya kocha mkuu, Luc Eymael, ilifanya mazoezi katika Uwanja wa Shule ya John Maelini jijini Dodoma ikiwa ni siku moja tu baada ya kurejea kutoka Shinyanga ilipocheza na Mwadui FC.

Yanga inaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa bao 3-2 katika mzunguko wa kwanza hivyo leo imepania kuendeleza ubabe katika mchezo huo utakaopigwa dimba la Jamhuri Dodoma.

Akizungumzia mechi hiyo, kocha msaidizi Charles Boniface Mkwasa alisema, wapo tayari kupambana na wapinzani wao na wamejiandaa kupata alama tatu kwa kuwa ndio mipango yao kwasasa.

“Tumejianada vizuri, wachezaji wapo kwenye hali nzuri kwasasa tunachosubiria ni muda tu, naamini vijana watapambana kuhakikisha wanaendeleza wimbi la ushindi na kuzidi kutuweka kwenye nafasi nzuri zaidi,” alisema Mkwasa.

Yanga itaendelea kumkosa winga wao wa kimataifa kutoka Ghana, Bernad Morrison, katika mchezo wa pili mfululizo ambaye hakusafiri na timu huku taarifa zake zikiendeela kuzua sintofahamu klabuni hapo.

Yanga ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi baada ya kucheza mechi 28 na kujikusanyia pointi zake 54.Source link

Related Post

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *